Home » Tanzania » Sababu za kung'olewa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela

Sababu za kung'olewa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela

12 April 2016 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela na Katibu Tawala wa Mkoa huo Abdul Rashid Dachi, kufuatia mkoa huo kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa hauna watumishi hewa.

Rais Magufuli ametangaza kutengua uteuzi wa Viongozi hao wa Mkoa wa Shinyanga leo April 11 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, mara baada ya kupokea Taarifa ya Mwaka 2014/2015 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na kupokea hundi kifani ya Bilioni 6 kutoka Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotokana na kubana matumizi.

Rais Magufuli ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi hewa, aliamua kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi kufikia jana Aprili, 10 2016 imebaini kuwepo watumishi hewa 45 huku zoezi likiwa linaendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini.

>>>’Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?’:-Rais Magufuli

Rais Magufuli amesema baada ya kutengua uteuzi wake, Anne Kilango Malecela atapangiwa kazi nyingine.
Pamoja na hatua hiyo, Rais Magufuli ametaka wakuu wa mikoa yote wawafichue watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja, na ameagiza timu iliyofanya uchunguzi Mkoani Shinyanga itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma.

 alipowaapisha wakuu wa mikoa, Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kusimamia zoezi la kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya malipo ya mshahara, ambapo mpaka tarehe 31 Machi, 2016 Jumla watumishi hewa 5,507 walibanika.

Kati ya shilingi Bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili kulipa mishahara, kati ya shilingi Bilioni 53 na 54 zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa.

 

Ad