Home » Tanzania » Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha wakuu wa mikoa 25

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha wakuu wa mikoa 25

15 March 2016 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 15 Machi, 2016 amewaapisha wakuu wa mikoa 25, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Walioapishwa na Mikoa yao katika mabano ni Said Meck Sadiki (Kilimanjaro), Joel Nkaya Bendera (Manyara), Dkt. Rehema Jonathan Nchimbi (Njombe), Said Thabit Mwambungu (Ruvuma), Mhandisi Evarist Welle Ndikilo (Pwani), Magesa Stanslaus Mulongo (Mara), Amina Juma Masenza (Iringa), John Vianney Kitayomba Mongella (Mwanza), Halima Omary Dendegu (Mtwara), Daudi Felix Ntibenda (Arusha), Amos Gabriel Makalla (Mbeya), Jordan Mugirage Rugimbana (Dodoma) na Aggrey Deaisile Joshua Mwanri (Tabora).

Wengine ni Godfrey Weston Zambi (Lindi), Kebwe Steven Kebwe (Morogoro), Anne Kilango Malecela (Shinyanga), Anthony John Mtaka (Simiyu), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Zelote Steven Zelote (Rukwa), Paul Christian Makonda (Dar es salaam), Martine Reuben Shigela (Tanga), Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu (Kagera), Meja Jenerali Mstaafu Raphael Mugoya Muhuga (Katavi), Meja Jenerali Emmanuel Edward Maganga (Kigoma), Mhandisi Mathew John Mtigumwe (Singida).

Rais Magufuli pia amewaapisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa hapa nchini (TAKUKURU) Bw. Alphayo Japani Kidata na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Valentino Longino Mlowola

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mteule Luteni Mstaafu Chiku Galawa hakuapishwa leo kutokana na dharura ya  kikazi, na tarehe ya kuapishwa kwake itapangwa siku nyingine.

Mara baada ya kukamilika kwa kiapo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa ujumbe kwa Wakuu wote wa Mikoa, ambapo amewataka kwenda kufanya kazi kwa kujiamini na kujielekeza kutatua kero za wananchi.

Maagizo mengine ya Rais Magufuli ni pamoja na kuwataka wakuu hao wa mikoa kusimamia ulinzi na usalama katika mikoa yao, na Kuhakikisha watu wanafanya kazi hususani vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

"Haiwezekani Vijana wawe wanashinda vijiweni wanacheza pool, wakati wazee na akina mama wapo mashambani wanalima. Kawahimizeni wafanye kazi, wasipofanya kwa hiari walazimisheni kufanya kazi" Alisema Rais Magufuli

Agizo jingine la Dkt. Magufuli ni kuwataka kusimamia udhibiti wa fedha za umma katika halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji na ametoa siku 15 kwa halmashauri hizo pamoja na Wizara na Taasisi za Serikali kuondoa majina ya wafanyakazi hewa katika orodha za mishahara ya watumishi wa umma.

Rais Magufuli pia ametaka Wakuu wa Mikoa wakasimamie utekelezaji wa Elimu Bure ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha shule zina madawati na majengo ya kutosha.

Dkt. Magufuli amewasisitiza wakuu hao wa Mikoa kutosita kufanya maamuzi na kuchukua hatua haraka, huku akitaka wawasimamie ipasavyo wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, Makatibu Tarafa na Watendaji wa kata na Vijiji ili watekeleze wajibu wao na waache kuwaonea wananchi wa chini.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam

15 Machi, 2016    

Ad