Home » Tanzania » Tanzania na Saud Arabia zasaini makubaliano ya kushirikiana Kiuchumi

Tanzania na Saud Arabia zasaini makubaliano ya kushirikiana Kiuchumi

24 March 2016 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na wajumbe wa Serikali zote mbili wakishuhudia uwekwaji saini wa mkataba kuhusu Ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika nyanja za Uchumi, Biashara, Uwekezaji, Ufundi, Vijana na Michezo. Kwa upande wa Tanzania mkataba ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga (kulia) na Serikali ya Saudi Arabia iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Adel Al Jubair.

Waziri Mahiga na Waziri Al Jubair wakibadilishana mkataba mara baada ya kusainiwa

Mhe. Rais Magufuli akiagana na Waziri Al Jubair

Waziri Al Jubair akiagana na Waziri Mahiga mara baada ya kumaliza mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli na zoezi la uwekaji saini kukamilika. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mhe. Al Jubair, Waziri Mahiga, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Abdallah Kilima (wa kwanza kulia) na ujumbe uliombatana na Waziri Al Jubair. 
Picha na Reginald Philip.
 

Mfalme wa Saudi Arabia Mtukufu Salman Bin Abdulaziz Al Saud amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa nchi yake imeichagua Tanzania kuwa nchi ya kipaumbele katika mpango wake wa kuimarisha zaidi mahusiano na Afrika uliolenga kuendeleza na kukuza biashara, uwekezaji na kushiriki katika miradi ya maendeleo.

Ujumbe wa Mtukufu Salman Bin Abdulaziz Al Saud umewasilishwa kwa Rais Magufuli leo tarehe 24 Machi, 2016 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mheshimiwa Adel Al Jubeir Ikulu Jijini Dar es salaam.

Katika Salamu hizo pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania, Mfalme Salman Bin Abdulaziz Al Saud amesema Saudia Arabia imedhamiria kukuza zaidi mahusiano kati yake na Tanzania ili kuwaletea manufaa makubwa wananchi.

Kwa upande wake Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Mfalme wa Saudi Arabia kwa kumtumia ujumbe na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuiongoza Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali yake itafurahi kuona Saudi Arabia inashirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kati na barabara.

Maeneo mengine ambayo Rais Magufuli na Waziri Adel Al Jubeir wameyazungumzia ni ushiriakiano kati ya Tanzania na Saudia Arabia katika kuendeleza Elimu, Utalii, Bandari na miundombinu.

Pamoja na kufanya Mazungumzo hayo, Rais Magufuli pia ameshuhudia utiaji saini wa mkataba kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika nyanja za Uchumi, Biashara, Uwekezaji, Ufundi, Vijana na Michezo, ambapo kwa upande wa Tanzania mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Augustine Mahiga, na kwa upande wa Saudi Arabia umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mheshimiwa Adel Al Jubeir.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam

24 Machi, 2016

 

Ad