Home » Tanzania » Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 1.65/- kwenye vyuo vya walimu

Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 1.65/- kwenye vyuo vya walimu

29 February 2016 | Tanzania

'SERIKALI YATENGA SH. BILIONI 1.6/- VYUO VYA UALIMU"

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 1.65/- kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vya walimu hapa nchini.

Alitoa kauli hiyo (Jumamosi, Februari 27, 2016), wakati akizungumza na walimu na watumishi wa sekta ya elimu kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mtwara uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara.

"Serikali inatambua uhumimu wa mafunzo kwa vitendo katika vyuo vya ualimu ni kwa sababu hiyo mwezi huu wa Februari tumetoa sh. bilioni 1.65/- kwa vyuo vya ualimu 35 vya umma nchini ili kuwezesha wakufunzi na walimu wanafunzi kushiriki kikamilifu mafunzo kwa vitendo (Block Teaching Practice)," alisema huku akishangiliwa.

Alisema fedha hizo zinapaswa zitumike kulipia posho za kujikimu, nauli na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Mapema, akizungumza na mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuimarisha elimu na akawaonya wote wanaowaharibia elimu watoto wa kike.

 

"Tunataka watoto wa kike wasome wa Kitanzania wasome hadi elimu ya juu waje wawe watumishi wa umma hapo baadaye. Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake tukikumbuka kaulimbiu ya Mama Salma Kikwete ya kwamba 'Mtoto wa Mwenzio ni wako'," alisema.

 

"Yeyote atakayemharibia mtoto wa kike masomo kwa kumrubuni na chips au pipi ajiandae kwenda Lilungu, (gereza la mkoa wa Mtwara)", alisema.

 

 (mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, FEBRUARI 28, 2016.

 
Ad