Home » Tanzania » Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

28 April 2016 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, kufuatia kifo cha Mke wa Rais Mstaafu wa Kenya Mama Lucy Kibaki aliyefariki dunia tarehe 26 Aprili, 2016.

Mama Lucy Kibaki ambaye ni Mke wa Rais Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Mwai Kibaki amefariki dunia Jijini London nchini Uingereza, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Katika salamu hizo Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na kifo hicho na kuongeza kuwa Kenya imempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yake.

Kupitia kwako Rais wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta napenda kumpa pole nyingi Rais Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Mwai Kibaki, Familia yake, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huu mkubwa” Amesema Rais Magufuli.

Dkt. John Pombe Magufuli pia amemuombea marehemu Lucy Kibaki apumzishwe mahali pema peponi, Amina.

 

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam

26 Aprili, 2016

Ad