Home » Tanzania » Rais Dkt.Magufuli akiwa na Mkewe wameungana kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji ya kimbari

Rais Dkt.Magufuli akiwa na Mkewe wameungana kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji ya kimbari

07 April 2016 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wameungana na wananchi wa Rwanda kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 22 ya tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari yaliyosababisha vifo vya watu takribani milioni 1.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika eneo la Gisozi Mjini Kigali, yalipo makumbusho ya mauaji ya Kimbari ambapo Rais Magufuli na Mkewe wakiwa na mwenyeji wao Rais Paul Kagame wa Rwanda na Mkewe Mama Janeth Kagame wameweka shada la mauaji katika eneo walipouawa idadi kubwa ya wananchi wa Rwanda na pia wakawasha mwenge wa matumaini kwa walionusurika katika mauaji hayo na kwa Taifa zima la Rwanda.

Pamoja na kupata historia ya mauaji hayo ya kimbari, Rais Magufuli akiongozwa na mwenyeji wake Rais Kagame ametembelea jumba maalum lililohifadhi kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha, ambapo amepata maelezo kutoka kwa wahifadhi wa makumbusho hiyo, na pia kujioonea picha na mabaki ya mifupa na mafuvu ya binadamu waliouawa.

Akizungumza mara baada ya kutembelea jumba hilo la makumbusho Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na mauaji hayo na kusema tukio hilo halipaswi kurudia.

"Haitatokea tena, hatuwezi kubadilisha yaliyopita lakini tunaweza kubadilisha mambo ya sasa na yajayo, mauaji haya hayapaswi kutokea tena" Amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ambaye aliingia nchini Rwanda jana tarehe 06 April, 2016 ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aingie Madarakani Tarehe 05 Novemba, 2015 ameondoka Mjini Kigali jioni hii na kurejea Jijini Dar es salaam.

 

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Kigali

07 April, 2016

Ad