Home » Tanzania » Nyumba ya Mwl Nyerere iliyopo Magomeni Mtaa wa Ifunda Namba 62, ambayo aliishi hapo miaka ya 1950.

Nyumba ya Mwl Nyerere iliyopo Magomeni Mtaa wa Ifunda Namba 62, ambayo aliishi hapo miaka ya 1950.

27 January 2018 | Tanzania

Wizara ya Maliasili na Utalii kuikarabati nyumba ya Nyerere Magomeni-Dk Kigwangalla

Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla (MB) mapema leo Januari 26, 2018,amefanya ziara maalum katika Makumbusho ya Kumbukumbu ya Nyumba ya Mwl Nyerere iliyopo Magomeni Mtaa wa Ifunda Namba 62, ambayo aliishi hapo miaka ya 1950.

Dk. Kigwangalla ameweza kujionea mambo mbalimbali ndani ya makumbusho hayo huku pia akipokea maoni ya namna ya kufanyiwa maboresho ya kituo hicho ikiwemo ufinyu wa eneo la ofisi na maegesho kwa wageni wanaotembelea hapo.

"Nimefika hapa leo kujionea Kituo hichi ambacho ni kielelezo kikubwa cha Mwasisi wa Taifa letu. Hapa pana hazina kubwa na kituo hiki kina mambo mengi sana ya kumuenzi Baba wa Taifa. Kwa hali tuliookuta kwa kweli tutakaa na timu yangu kuona tunafanya maboresho makubwa kabisa ili kiwe kama maeneo mengine yenye Waasisi wa Mataifa yao, tumeona kama eneo alilozaliwa Mzee Mandela kule Afrika Kusini, nyumba yake imehifadhiwa vizuri na imekuwa na wageni wengi.

Kwa hapa kwetu na sisi tutakaa na wenzetu kutatua changamoto hizi. Hapa tutajenga Maktaba ambapo watu watakuja kusoma vitabu vya Mwasisi wetu na kuona mambo aliyokuwa akifanya. Lakini pia tutaonana na Viongozi wa Halmashauri ya Kinondoni kuona namna ya kupaboresha mahala hapa ikiwemo miundombinu ya Barabara ya kuingia na kutoka eneo ili" alieleza Dk. Kigwangalla.

Pia aliongeza kuwa, kituo hicho kipo katika hali mbaya kikikabiliwa na changamoto  licha ya kuwa ni kituo muhimu sana hapa nchini. 

Hivyo amewahakikishia wahifadhi wa Makumbusho hayo mipango iliyopo ni pamoja na kukifanyia marekebisho kwa kutengeneza choo, kukipaka rangi pamoja na kukifanyia ukarabati mkubwa.

Aidha, amesema kuwa, lengo kwa sasa ni kuifanya nyumba hiyo iwe kama nyumba halisi ailivyokuwa akiishi mwenyewe Baba wa Taifa kwani ndani bado kuna vitu halisi alivyokuwa akivitumia Mwasisi mwenyewe huku pia mikakati ni pamoja na kununua hata nyumba za jirani ili kuongeza eneo na kuongezwa baadhi ya ofisi na pawe na hadhi kama Mwasisi mwenyewe" alieleza Dk.Kigwangalla.

"Kiukweli nimefika hapa kushuhudia makumbusho haya ambayo kiuhalisia hapa ni hazina kubwa sana ya kumbukumbu ya Taifa letu hasa katika harakati za kupigania Uhuru pia zilianzia hapa katika nyumba hii. Pia tutaboresha zaidi kwa kuweka studio maalumu ambayo pia tutaboresha CD zote za Baba wa Taifa zitakuwa zikioneshwa humo ikiwemo zile za Hotuba.

Awali Muhifadhi Mkuu wa Makumbusho hayo, Bi. Neema Mbwana alieleza changamoto zinazoikabili kituo hicho pamoja na kuomba kuboreshwa kwa vitu muhimu ikiwemo Ukarabati wa nyumba nzima kuanzia paa na kupaka rangi.

Mhifadhi huyo aliendelea kusema kuwa, kwa umuhimu wa vitabu ambavyo hakuna nakala zake halisi ambavyo ni mali za Baba wa Taifa, walimuomba Waziri awachapishie tena nakaza zaidi ili ziweze kutumika kwa miaka mingi zaidi kwani vilivyopo vimechakaa.

Mbali na kutembelea Makumbusho hayo ya Nyumba ya Baba wa Taifa hiyo ya Magomeni, Dk. Kigwangalla pia aliweza kutembelea eneo la wachoraji wa michoro ya Tingatinga yaliyopo Oysterbay pamoja na soko kubwa la Vinyago lililopo Mwenge na kujionea wachongaji vinyago ambao ni kiungo muhimu cha Utalii hapa nchini hata hivyo alikutana na kero juu ya Watalii kusumbuliwa Viwanja vya ndege kwa bidhaa zao hizo za vinyago.