Home » Tanzania » Muhongo, ameiomba Norway kuisaidia Tanzania kupitia mafunzo ya uchimbaji wa gesi,mafuta

Muhongo, ameiomba Norway kuisaidia Tanzania kupitia mafunzo ya uchimbaji wa gesi,mafuta

07 January 2016 | Tanzania

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri  wa Nishati na Madini Profesa Sospter Muhongo,  ameiomba nchi ya Norway kuisaidia  Tanzania kupitia mafunzo  hususan katika utafutaji na uchimbaji wa gesi  na mafuta ili kuongeza wataalam wa gesi na mafuta nchini.

Profesa Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake na balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad aliyeambatana na ujumbe wake uliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam.

Kikao hicho pia kilishirikisha watendaji  kutoka Wizara ya Nishati na Madini ambao ni  pamoja na Naibu Katibu Mkuu- Nishati, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo, Naibu Katibu Mkuu- Madini Prof. James Mdoe.

Aidha,  kikao hicho kilishirikisha watendaji kutoka katika taasisi zilizopo chini ya Wizara  ambazo ni pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Jiolojia  Tanzania (GST) na  Wakala wa  Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA)

Profesa Muhongo alisema kuwa sekta mpya ya  utafiti na uchimbaji wa  gesi na mafuta inahitaji wataalam zaidi na kuongeza kuwa serikali imekuwa ikiwapeleka wataalam wake   kwenda kusomea masuala ya gesi na mafuta katika  vyuo vilivyoko nje ya nchi  kama Scotland na Uingereza.

Alisema kuwa serikali imeanzisha kozi  katika   Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Chuo cha Madini  Dodoma.

“ Bado tuna uhitaji mkubwa wa wahadhiri  wenye  Shahada za Uzamifu (PhD) kwa ajili  ya kufundisha katika  vyuo vyetu, na kuzalisha wataalam  watakaofanya kazi katika makampuni  yanayojishughulisha na  utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini.

Akielezea kuhusu  hali ya umeme nchini Profesa Muhongo alisema kuwa hali ya umeme nchini ni nzuri kutokana na serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika.

Alisema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Nishati  Vijijini  imekuwa ikisambaza nishati ya umeme vijijini pamoja na kutoa ruzuku kwa  wazalishaji umeme mdogo kwa njia ya maji (min-hydro) na kuitaka Norway kuisaidia REA ili iweze kufanikisha miradi yake.

Akielezea changamoto katika uzalishaji wa umeme nchini Profesa Muhongo alisema  ipo mitambo ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji yenye kuhitaji matengenezo na kuiomba serikali ya Norway kusaidia matengenezo ya mitambo hiyo.

Aliongeza changamoto nyingine ni vyanzo vya maji kutosimamiwa ipasavyo katika mabwawa ya maji  ya kuzalishia  umeme na kusisitiza kuwa  tayari serikali imeanza kufanyia kazi changamoto hiyo.

Naye Balozi wa Norway Nchini Hanne-Marie Kaarstad alisema kuwa serikali ya Norway  imekuwa na  ushirikiano mzuri na serikali ya Tanzania katika sekta ya nishati na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.

Ad