Home » Tanzania » Mhe. Mbarawa ametengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme

Mhe. Mbarawa ametengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme

19 February 2016 | Tanzania

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame Mbarawa ametengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Marcellin Benedict Magesa kuanzia Februari 18 mwaka huu.

Profesa Mbarawa amechukua hatua hiyo kutokana na kuwepo kwa sababu mbalimbali zikiwemo, kushindwa kusimamia matengenezo ya magari na mitambo ya Serikali nchini, kushindwa kusimamia uendeshaji wa matenegenzo ya vivuko vya Serikali nchini pamoja na kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo mbalimbali.

‘’Mhandisi Marcellin Benedict Magesa atapangiwa majukumu mengine wizarani Na hivyo namteua Mhandisi Manase Lomayani Le-Kujan kuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuanzia Leo hii ’’, alisema Profesa Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa amemuagiza Kaimu Mtedaji Mkuu huyo aliomteua kutekeleza mara moja mambo mbalimbali, ikiwemo kutengeua uteuzi wa Mkurugenzi anayeshughulikia matengenezo ya magari ya Serikali, Mhandisi Prisca Benedict Mukama na kumpangia majukumu mengine, pia kutengua uteuzi wa Meneja wa Karakana ya Magari ya Serikali (M.T Depot), Mhandisi John Alexander Mushi na kumpangia majukumu mengine.

Kabla ya uteuzi wake, Mhandisi Manase Lomayani Le-Kujan alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Ufundi na Ushauri katika Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Ad