Home » Tanzania » Mawaziri watakiwa kujaza fomu za maadili leo kabla ya saa 12 jioni

Mawaziri watakiwa kujaza fomu za maadili leo kabla ya saa 12 jioni

26 February 2016 | Tanzania

Baadhi ya Mawaziri na Manaibu Waziri wasiorudisha   fomu za  Tamko la Rasilimali na Madeni na fomu ya Ahadi ya Uadilifu  wamesisitizwa kurudisha fomu hizo  leo kabla ya saa 12 jioni  katika  ya Ofisi ya Tume ya Maadili iliyopo jijini  Dar es salaam na watakaoshindwa kufanya hivyo watakua wamejitoa wenyewe kwenye nafasi zao.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ofisini kwake alipokutana na Waandishi wa Habari akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah  Kairuki.

Alieleza kuwa kufuatia Semina  iliyofanyika Februari 25 mwaka huu kati yake na  Mawaziri kuhusu  mwongozo wa maadili ya viongozi wa Umma na utekelezaji wa ahadi ya uadilifu, ambapo Kamishna Mkuu Jaji Mstaafu Salome Kaganda alitoa maelezo kwamba kuna baadhi ya Mawaziri na Manaibu Waziri ambao hawajarudisha fomu hizo hadi kufikia jana.

Viongozi ambao hawajarudisha fomu hizo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Charles Kitwanga, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano, January Makamba, ambao wote hawajarudisha fomu za rasilimali na madeni na fomu za ahadi ya uadilifu, vilevile  Waziri wa Mambo ya nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Augustine Mahiga ambaye  hajarudisha fomu ya Ahadi ya Uadilifu.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako ambaye  hajarudisha fomu ya tamko la rasilimali na madeni pamoja na naibu waziri ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano Luhaga Mpina ambaye hajarudisha fomu zote mbili.

Waziri mkuu Majaliwa amewasisitiza mawaziri hao kujaza fomu hizo kwa kua ni agizo la Mheshimwa Rais kujaza fomu hizo leo kabla ya saa 12 jioni, “viongozi watakaoshindwa  kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni  na fomu ya Ahadi ya Uadilifu wanatakiwa kujieleza kwa kutoa sababu za kushindwa kufanya hivyo na watachukuliwa hatua”

Kwa mujibu wa kifungu cha 9 Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma ya mwaka 1995 sura ya 8 inawataka viongozi wote wa umma kujaza fomu za kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma (Tamko la Raslimali na Madeni) na fomu ya Ahadi ya Uadilifu mara wanapoteuliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Lengo la kujaza fomu hizo ni kuwa na uwajibikaji kwa kiongozi juu ya uadilifu wake wakati wote anapokua mtumishi wa Umma.

Ad