Home » Tanzania » Eneo la Ekari 109 kutumika kujenga hospitali ya Uhuru jijini Dodoma

Eneo la Ekari 109 kutumika kujenga hospitali ya Uhuru jijini Dodoma

18 January 2019 | Tanzania

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua eneo la ujenzi wa hospitali ya Uhuru lenye ukubwa wa ekari 109 lililoko katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Maduma wilayani humo leo mchana (Ijumaa, Januari 18, 2019), Waziri Mkuu amesema uamuzi wa Serikali ya kijiji hicho wa kutenga maeneo ya maendeleo ni wa kupigiwa mfano na vijiji vya maeneo mengine.

 

 
“Uamuzi wenu wa kutenga maeneo ya miradi ya maendeleo umekuwa na tija, ndiyo maana Mheshimiwa Rais Magufuli aliposema ijengwe hospitali, hamkupata shida sababu eneo tayari lilikuwepo. Ninawapongeza wazee waliojitolea maeneo yao ili kuongeza kwenye eneo la hospitali,” amesema.
 
Wazee waliotoa maeneo yao ni Mzee Meshack Njamasi (ekari 5.50), Mzee Jobu Malogo (ekari 3.50) na Bw. Nehemia Mwikwi (ekari 4.50). Ekari 95.5 zilizobakia, zimetolewa na Seriakli ya kijiji hicho.
 
Waziri Mkuu aliwataka wakazi wa wilaya ya Chamwino wasibweteke bali wajipange na kila mmoja ajipange kufanya kazi kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa akihimiza. “Ujenzi wa mji wa Serikali unaoendelea hivi sasa ni fursa kwenu. Na ujio wa hospitali hii ni fursa nyingine kwa wana-Chamwino hasa kwa vile ujenzi wake utatumia mfumo wa force account ambao unatoa fursa kwa wanajamii kushiriki kazi za miradi ya eneo husika,” amesema.
 
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa hospitali hiyo yenye hadhi ya wilaya ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoelekeza wananchi wapatiwe huduma za matibabu huko huko waliko. “Hadi sasa tumeshajenga vituo vya afya 350 ili kusogeza huduma kwa wananchi na jumla ya hospitali za wilaya 67, zinajengwa nchi nzima kwa mwaka huu,” amesema.
 
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakazi wa vijiji jirani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Bw. Selemani Jafo alisema eneo la ujenzi wa hospitali hiyo liko umbali wa kilometa mbili kutoka barabara kuu ya Dar es Salaaam-Dodoma na kilometa tatu kutoka Ikulu ya Chamwino.
 
Naye, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine aliwataka wakazi hao wachangamkie fursa hiyo kwa kusomba mawe, mchango, maji na kwamba Kamati za usimamizi wa ujenzi zitapaswa kusimamiwa na wanakijiji.
 
Aliwataka wakazi hao wasiishie kwenye lengo la kuwa na hospitali ya wilaya, bali walenge kujenga hospitali yenye hadhi ya mkoa kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.
 
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni wa hadhi ya wilaya ikiwa na nyongeza ya huduma za wagonjwa wa dharura na wagonjwa mahututi (Emergency Department and Critical Care Unit).
 

Alimshukru Rais Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa hospitali hiyo sh. milioni 995.18 ambazo zilipaswa kutumika kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru, Desemba 9, mwaka jana. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuongezea kiasi kingine cha fedha cha sh. bilioni 2.35 na kutufanya sasa tuwe na sh. bilioni 3.22 za ujenzi huo,” alisema.

 
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge  (kulia) wakati alipokagua eneo itakapojengwa Hospitali ya Uhuru katika kijiji cha Maduma wilayani Chamwino, Januari 18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha michoro ya majengo ya Hospitali ya Uhuru inayotarajiwa kujengwa katika  kijiji cha Maduma wilayani Chamwino wakati alipokagua eneo hilo, Januari 18, 2019. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo (katikati) na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile wakati alipokagua eneo itakapojengwa  Hospitali ya Uhuru katika kijiji cha Maduma wilayani Chamwino, Januari 18, 2019.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimshukuru Mzee, Meshack Njamasi, mmoja wa wananchi waliotoa maeneo yao bure kwa serikali ili yatumike kwa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru katika kijiji cha Maduma wilayani Chamwino, Januari 18, 2019. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimshukuru  Mzee,  Job Mahogo, mmoja wa wananchi waliotoa maeneo yao bure kwa serikali ili yatumike kwa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru katika kijiji cha Maduma wilayani Chamwino, Januari 18, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

Ad