Home » Biashara » Serikali yaimarisha Mazingira ya Uwekezaji-Kairuki

Serikali yaimarisha Mazingira ya Uwekezaji-Kairuki

12 February 2019 | Biashara
 
Na Grace Semfuko-MAELEZO 
 
Serikali imeweka mpango wa kuboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi mpango unaolenga kurahisisha vibali na upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Viwanda na maeneo ya Kilimo. 
 
Hayo yamebainishwa Jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye makao makuu ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, baada ya kupokea ujumbe wa raia saba wa Hongkong China waliowasili Nchini wakiwawakilisha wafanyabiashara wa nchi hiyo waliokuja kufanya utafiti wa maeneo ya kuwekeza. 
 
Waziri Kairuki alisema hivi sasa Wizara yake iliyopo Chini ya Waziri Mkuu imeanza kuufanyia kazi mpango huo ambapo pamoja na kuimarisha uchumi wa Nchi kwa kuingiza fedha za kigeni pia utaongeza ajira kwa watanzania. 
 
“Sisi kama Serikali lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaimarisha uwekezaji, mpango huo ambao ulifanyika mwezi Mei mwaka jana unalenga kuondokana na vikwazo vya kibiashara na kuharakisha vibali na kutoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji, tunayafanya haya ili kuongeza ufanisi katika sekta ya uwekezaji, tunataka Watanzania wanufaike” alisema Angellah Kairuki. 
 
Alisema mwaka 2018 mwezi Mei Serikali iliweka mkazo katika andiko la mpango wa kuboresha biashara na uwekezaji pamoja na mpango mkakati wa kuhakikisha kuondoa vikwazo vya biashara mpango ambao unafanikiwa kwa kiwango kikubwa. 
 
Nae Jessica So ambaye ni Mwakilishi wa Balozi wa Heshima wa Tanzania Hongkong alisema lengo la ujio wao ni kufanya utafiti wa maeneo ya uwekezaji na kibiashara ambapo wanaanza kwa kuangazia maeneo manne yaliwepo ya Sekta ya Dawa, Kilimo cha Ufuta na Korosho pamoja na Sekyta ya Utalii. 
 
“Sisi ni ujumbe wa watu saba kutoka Hongkong China, tumekuja hapa kuangalia ni kwa namna gani tutashirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye maeneo manne ya Dawa, Ufuta,Korosho na Utalii, tunawawakilisha wafanyabiashara wengine na tutawapelekea ujumbe wa tutakayoyaona hapa Tanzania” alisema Mwakilishi wa Wajumbe hao Jessica So Raia wa HongKong China. 
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Geoffrey Mwambe alisema tayari walishafanya mazungumzo na Mamlaka ya maendeleo ya biashara Hongkong ambayo inashughulikia biashara na uwekezaji kusaini makubaliano ya kuhakikisha wafanyabiashara wengi wanatumia fursa zilizopo Hongkong na Tanzania. 
 
Ujio wa Wajumbe saba kutoka Hongkong Nchini China ni sehemu ya wafanyabiashara wengi kutoka Jijini humo wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania hatua ambayo imekuja kufuatia kuwepo kwa hamasa ya uwekezaji na kuimarishwa kwa mazingira hayo nchini.
Ad