Home » Biashara » Serikali imetoa agizo kwa watendaji wa Kituo cha pamoja cha Forodha Mpakani- Horohoro

Serikali imetoa agizo kwa watendaji wa Kituo cha pamoja cha Forodha Mpakani- Horohoro

12 February 2019 | Biashara
 
 
Na Peter Haule,
WFM, Tanga
 
Serikali imetoa agizo kwa watendaji wa Kituo cha pamoja cha Forodha Mpakani- Horohoro, kuwasilisha nyaraka za ujenzi wa Kituo hicho ukiwemo mkataba kwa kuwa miundombinu iliyopo haijakidhi viwango jambo lililosababisha kutofunguliwa rasmi kwa kituo hicho tangu mwaka 2015.
 
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro walipofanya ziara ya kutembelea na kukagua Kituo hicho ambapo hawakuridhishwa na miundombinu yake.
 
Dkt. Kijaji, alisema kuwa Kituo hicho hakina mawasiliano kati ya upande wa Tanzania na Kenya hivyo kutokidhi vigezo vya kuwa Kituo cha pamoja cha Forodha kati ya nchi hizo mbili.
 
Alisema kuwa ukosefu wa mawasiliano unasababisha urasimu katika kuwahudumia wananchi jambo linalosababisha wateja katika mpaka huo kutafuta njia nyingine ambazo sio rasmi katika usafirishaji bidhaa jambo ambalo linaathari kubwa katika ukusanyaji wa mapato.
 
Miongoni mwa kasoro zilizobainika wazi ni kamera maalum za usalama zinazotakiwa kufanyakazi ni zaidi ya 14 lakini zinazofanyakazi mpaka sasa ni 4 pekee jambo linalotiashaka kuhusu usalama wa Kituo hicho
 
Dkt. Kijaji, alisema pia, utaratibu wa wakazi wa Horohoro kwenda kupata huduma za TRA katika Wilayani Muheza usitishwe na badala yake watumishi wa Mamlaka hiyo waende kuwahudumia wananchi katika Wilaya ya Mkinga ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara wanapotaka kulipa kodi au kutafuta huduma za masuala ya forodha.
 
Aidha, Manaibu Waziri hao wameiagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Tanga kuhakikisha Jenereta la Kituo hicho cha Pamoja cha Forodha linafanyakazi ndani ya saa 24 ili kukabiliana na upotevu wa mapato katika eneo hilo kinyume na hapo hatua zingine zitachukuliwa.
 
Manaibu Waziri hao wametoa maagizo hayo baada ya kuelezwa kuwa jenereta halifanyikazi baada ya kuharibika kwa takribani siku 14 na kusababisha Seikali ikose mapato na kuleta usumbufu kwa watumiaji wa Kituo hicho kwani hulazimika kukaa muda mrefu kusubiri umeme urejee baada ya kukatika.
 
“Kutofanya kazi kwa Jenereta katika Kituo cha Forodha- Horohoro kumechangia kukosekana kwa kumbukumbu sahihi ya magari yanayopitisha bidhaa katika mpaka huo hivyo kuwa na athari katika takwimu za mapato ya eneo hilo lakini pia usalama wa Taifa”. Alisema Dkt. Kijaji
 
Viongozi hao wameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kutengeneza skana ya kuchunguza usalama wa mizigo na wateja wanaoingia kwenye Kituo hicho ambayo imeharibika muda mrefu hali inayohatarisha usalama wan chi, raia na mali zao
 
Kwa upande wake Dkt. Ndumbaro, ameagiza kuchimbwa kwa kisima cha maji eneo hilo kwa kuwa kiasi cha Sh. milioni sita kinachotumika kuagiza maji kila mwezi kinaweza kutumika kujenga kisima cha kudumu na kuokoa fedha nyingi zisipotee.
 
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Damas Ndumbaro wapo katika ziara mkoani Tanga na maeneo mengine katika kutatua changamoto za ukusanyaji wa mapato na suala la usalama katika mpaka wa Tanzania na Kenya.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro na  Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakikagua Scana katika Kituo cha pamoja cha Forodha katika eneo la Horohoro Mkoani Tanga ambayo ilikuwa haifanyi kazi kwa kukosa umeme jambo lilololeta shaka kwa usalama bidhaa zinazoingia na kutoka nje ya nchi.
 Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga Bi. Specioza Owure, akifafanua jambo wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt.Damas Ndumbaro na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), walipotembelea na kukagua Kituo cha pamoja cha Forodha katika eneo la Horohoro Mkoani Tanga.
 Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga Bw. Yona Mark, akieleza Changamoto za Kituo cha pamoja cha Forodha katika eneo la Horohoro ambazo ni pamoja na  kuwepo kwa njia nyingi zisizo rasmi za upitishaji wa bidhaa kutoka Tanzania na Kenya, jambo ambalo linaikosesha nchi Mapato. 
 Afisa Mfawidhi wa  wa Mamlaka ya Mpato Tanzania Kituo cha pamoja cha Forodha katika eneo la Horohoro mkoani Tanga, Bw. Bakari Athuman, akitoa ufafanuzi wa changamoto za ukusanyaji mapato katika Kituo hicho wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Kituoni hapo.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Damas Ndumbaro (kulia), wakihoji namna ambavyo Kituo cha pamoja cha Forodha - Horohoro  kinavyotunza kumbukumbu za vyombo vya moto vinavyoingia na kutoka, kwa kuwa hawakuridhika na idadi ya magari ambayo yalipita kwa siku mbili, jambo lililotia shaka ukusanyaji wa mapato Kituoni hapo. Katikati ni Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji  Kituo cha pamoja cha Forodha - Horohoro Bw. Antony Kasitu.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Dkt. Damas Ndumbaro, wakikagua nmyaraka mbalimbali na kutoa agizo la kuboresha kumbukumbu ili kulisaidia Taifa katika suala la ukusanyaji wa mapato na usalama.
Mhandisi wa Mifumo ya Tehama wa Kituo cha pamoja cha Forodha – Horohoro, Mossy Mundonko,  akieleza changamoto ya kutokuwepo kwa mawasiliano kati ya upande wa Tanzania na Kenya jambo linalosababisha kushuka kwa ufanisi wa Kiutendaji wa Kituo hicho, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro wakatoa maagizo ya kupelekwa makataba wa ujenzi wa Kituo hicho kabla ya hatua zingine kuchukuliwa.
 (Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)
Ad