WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) ameongoza ujumbe maalum wa Tanzania kwenye mkutano wa tatu wa Dunia wa Utalii na Utamaduni,
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) ameongoza ujumbe maalum wa Tanzania kwenye mkutano wa tatu wa Dunia wa Utalii na Utamaduni, ambao ni mkutano wa juu zaidi wa sera za utalii unaofanyika kila mwaka.
Katika mkutano huo wa siku tatu, Desemba 3-5, 2018,umeandaliwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya likiwemo Shirika linalosimamia Utalii (UNWTO) na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambapo Mawaziri na watunga sera zaidi ya 300 wanakutana jijini Istanbul, Uturuki, kuzungumzia mambo mbali mbali yanayohusu utalii wa utamaduni.
Waziri Dkt. Kigwangalla amepata fursa ya kuzungumza kama mmoja wa wanajopo Mawaziri wa Utalii wa nchi wanachama na kuzungumzia faida za utamaduni katika kuvutia watalii kwa kuelezea uwepo wa makabila mengi Tanzania.
“Tanzania imejaaliwa kuwa na makabila zaidi ya 128 yanayoongea lugha mbalimbali, pengine ni nchi yenye makabila tofauti tofauti zaidi ya nchi yoyote ile afrika na pengine duniani, lakini imefanikiwa kuunganishwa na lugha moja, na utamaduni mmoja wa kiswahili, ambacho ni zao la mila na desturi mchanganyiko za makabila hayo.
Wageni wa Kireno, Kiarabu, kihindi, kigiriki, kijerumani na kiingereza. Wageni hawa walikuja kufanya biashara na watu wetu, kutangaza dini ama kutawala!” Amesema Dkt. Kigwangalla katika mkutano huo.
Adiha, Dkt. Kigwangalla ameongeza kuwa, Utamaduni unaishi, unaendelea na unabadilika kila wakati, lakini pamoja na changamoto hizo na nia yetu ya kutaka kuleta maendeleo na teknolojia za kisasa kwa watu wetu, tuna jukumu la kulinda na kuhifadhi utamaduni, mila na desturi zetu na kurithisha vizazi vijavyo, vinginevyo tutapoteza urithi wetu na namna pekee ya utambulisho wetu wa kipekee!.
“Nchini kwetu Tanzania tuna changamoto kubwa ya kulinda lugha zote nne zinazopatikana Afrika.Kwa kuwa sisi ni nchi pekee Afrika ambayo ina ndimi zote zinazozungumzwa Afrika; tuna Wabantu, Wahamitiki/Wakushtiki, Wanilotiki na Wasandawe/Wahadzabe. Kwa mfano Wahadzabe wamebaki kama 1000 au 2000 hivi kwa ujumla wake, na ni kivutio cha kipekee cha Utalii kwa sababu bado wanaishi maisha kama walivyoishi wahenga wao” amebainisha Dkt. Kigwangalla katika mkutano huo.
Aidha, pamoja na kutaka kuutumia utamaduni wa watu kwa ajili ya kukuza shughuli za utalii, mkutano huu umesisitiza kuheshimu utamaduni, mila na desturi za watu kwa malengo ya kuhifadhi na kuulinda na kupunguza kutumia vivutio kupita kiasi ili kuwa na utalii unaoendana na maendeleo endelevu.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara hiyo ya Maliasili na Utalii imeanzisha mwezi maalum wa kusherehekea Urithi wa Mtanzania kupitia tamasha la Urithi Festival ambalo litafanyika kila mwaka mwezi wa Tisa kwa nia ya kuutumia utamaduni wetu kuleta kipato kwa wananchi, kuchachua uchumi na kuutangaza kwa wageni na hatimaye kuboresha ‘experience’ wanayopata watalii wanapokuja nchini.
Katika hatua nyingine Dkt. Kigwangalla amesema Serikali ya Tanzania inawashirikisha wananchi wa jirani na maeneo ya utalii kuuza bidhaa na kufanya maonesho ya bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuunganisha utalii na maisha ya watu.
Pamoja na mkutano huo, Dkt.Kigwangalla amefanya mikutano ya ana kwa ana na Mawaziri mbalimbali katika jitihada za kuanzisha mahusiano ya kutangaza vivutio vya nchi husika miongoni mwa Mawaziri aliofanya mazungumzo hayo ni Waziri wa Utalii na Utamaduni wa Oman, China, Jamaica na Meya wa Jiji la Kyoto ambako mkutano wa mwakani utafanyikia.
Pia amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa la mambo ya Utalii, Bwana Zurab Pololikashvili.