WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Temeke kutoa ajira
WAZIRI MKUU ATOA SIKU MOJA KWA HALMASHAURI YA WILAYA TEMEKE KUMALIZA TATIZO LA AJIRA ZA MIKATABA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Temeke kuondoa wafanyakazi wa mkataba kwa kuwapa ajira ya kudumu ifikapo Julai 30 mwaka huu.
Amesema kitendo cha kutowaajiri na kuwatumikisha kwa mikataba kwa muda mrefu kinasababisha wakose stahiki zao jambo ambalo si halikubaliki.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Julai 28, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo na kusisitiza kwamba ni lazima sula hilo lishughulikiwe haraka kwa sababu hayo ndio matundu watumishi hewa.
“Mnawatumikisha watu kama vibarua kwa muda mrefu, hapa kuna wengine wanafanya kazi kwa mikataba kwa miaka mitano hadi sita hii haikubaliki kwani mnawakosesha stahili zao pale mnapowaachisha kazi,” amesema.
Awali Kaimu Ofisa Utumishi wa Manispaa hiyo Zaitun Hassan alisema wamekuwa wakitoa ajira za mikataba kwa sababu wamekosa watu wenye sifa za kuweza kuajiriwa husan madereva.
“Kwa mara ya mwisho umetangaza lini nafasi za ajira? Katika mkoa wa Dar es Salaam kweli wanaweza kukosekana madereva wenye sifa za kuajiriwa? Alihoji Waziri Mkuu.
Zaitun alisema kuwa madereva wengi wanaojitokeza pindi wanapotangaza ajira wanashindwa kufikia vigezo ikiwemo kuwa na cheti cha VETA na badala yake wanakuwa na cheti cha kidato cha nne tu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kuwa kuna wafanyakazi wengine katika Idara ya Uhasibu na Ujenzi ambao nao wameajiriwa kwa mkataba hivyo amemtaka Ofisa Utumishi kuomba kibali cha kuajiri kwa Katibu Mkuu Utumishi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufanya tathmini ya maeneo yote ya shule kwenye mkoa wake na watakaobainika kuingia katika maeneo hayo waondolewe haraka.
Amesema baada ya kukamilisha utengenezaji wa madawati kinachofuatia sasa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambapo amezitaka halmashauri kuweka mipango ya kujenga majengo ya madarasa ya ghorofa ili waweze kuwa na madarasa mengi katika eneo dogo.
Awali Waziri Mkuu alipokea msaada wa madawati 705 katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Chamazi wilayani Temeke ambapo kati yake Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania umetoa madawati 600 na Jumuia ya Mabohora imetoa madawati 105.
Pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Agustino Mahiga alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 85 fedha zilizochangwa na watumishi wa wizara hiyo kwa ajili ya kuchangia utengenezaji wa madawati.
Dk. Mahija alisema watumishi hao walichanga sh. milioni 100 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati ambapo sh. milioni 15 wamekabidhi kwa mkuu wa wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe ambaye alikuwa mtumishi wa wizara hiyo ili naye akatengeneze madawati kwa shule za wilayani kwake.
Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini Jaseem Al Najem amesema Serikali ya Kuwait itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika shughuli zote za maendeleo hususan katika sekta za elimu na afya.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, JULAI 28, 2016