WANAHABARI SACCOS Kuanzishwa Tanzania
Wanahabari nchini Tanzania wameungana ili kuanzisha “WANAHABARI SACCOS” katika mkutano wao wa kwanza wa maandalizi uliofanyika leo 29May2016 jijini Dar es salaam Katika Mgahawa wa City Sports Longe mkabala na mnara wa askari Posta.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe wasiopungua Ishirini na wawili, WANAHABARI SACCOS inadhamiria Kuinua, kustawisha na kuboresha hali ya uchumi na kijamii kwa Wanahabari wanachama, kwa kuwahamasisha kuchukua mikopo yenye manufaa na riba nafuu pamoja na huduma nyingine za kifedha kwa kutumia mfumo wa kisasa.
Baadhi ya Sifa ili kujiunga na WANAHABARI SACCOS ni lazima uwe na sifa zifuatazo:- Awe mwenye umri usiopungua miaka kumi na nane (18). Awe ni Mwanahabari aliye katika Tasinia ya Habari, Awe mwenye tabia nzuri, mwaminifu na akili timamu, Awe amelipa kiingilio, hisa na kuweka akiba kwa kiwango kilichowekwa kwa mujibu wa masharti haya na awe tayari kushiriki kikamilifu shughuli za chama zinazompasa.
Awe tayari kufuata Masharti ya chama, sheria ya Vyama vya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na kanuni zake wakati wowote.
Katika kupokea wanachama, WANAHABARI SACCOS itapokea wanachama kwa kuzingatia uwazi na hiari bila kujali itikadi za kisiasa, kidini, kijinsia au ubaguzi wa kijamii bali yeyote awezaye kuchangia na kuhitaji huduma zitolewazo na chama.
WANAHABARI SACCOS itachochea mipango ya utoaji elimu kwa wanachama, viongozi na watendaji wake ili kila mmoja aweze kijifunza kutoka kwa mwingine na kuweza kufundishana wenyewe kwa wenyewe katika kutimiza wajibu wao.
WANAHABARI SACCOS itaelimisha wanachama wake kuhusu uendeshaji na manufaa ya SACCOS. Wazo la kuanzisha WANAHABARI SACCOS limeanzia katika Mtandao wa kijamii wa WhatsApp la 'TASINIA YA HABARI' lenye waandishi wa Habari 256, hata hivyo "Group" hili linatarajiwa kuongeza wanachama zaidi.