Vijana hawajajengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika - Waziri Mkuu
22 April 2016 | Tanzania
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana nchini kimepungua kwa asilimia 2.5 na kwamba Serikali itaendeleza juhudi za kuvutia uwekezaji ili kupunguza zaidi kiwango hicho.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Aprili 22, 2016) wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.
“Utafiti wa hali ya ajira nchini wa mwaka 2014 umeonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3 mwaka 2014. Aidha, ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014,” amesema.
Waziri Mkuu amesema moja ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira ni vijana kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi Nchini (2015/2016 – 2019/2020).
“Programu hiyo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi kutoka asilimia tatu ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha uchumi wa viwanda. Vilevile, kupunguza idadi ya watu wenye kiwango cha ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 54,” amesema.
Amewaagiza watendaji wakuu wa wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali, taasisi za umma, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha kuwa ukuzaji wa ajira unakuwa ni agenda ya msingi ya kudumu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumzia kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu hususan watu wenye ualbino, Waziri Mkuu amesema Serikali inafanya jitihada kubwa kukomesha vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwakamata wote wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Ukatili huo umesababisha watu wenye ualbino kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu. Hali hiyo haikubaliki na haivumiliki katika jamii ya Watanzania. Napenda kusisitiza watu wenye ulemavu wana haki ya kuthaminiwa utu wao na kulindwa dhidi ya ukatili na aina yoyote ya ubaguzi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaviboresha Vyuo vya Ufundi na Marekebisho (Vocational and Rehabilitation Training Centres) vya watu wenye ulemavu nchini ili kutoa ujuzi unaoendana na mahitaji yao katika soko la ajira ikiwa ni pamoja na kuandaa walimu wa elimu maalum na kutoa vifaa saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye ulemavu mashuleni.
Akitoa maelezo kuhusu juhudi za Serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi, Waziri Mkuu amesema Serikali imesaidia uanzishwaji wa taasisi mwavuli ya kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA ambayo imeanza kuonyesha matunda mazuri.
“Takwimu zilizotolewa mwezi Februari 2016 na taasisi hiyo zinaonesha kuwa kuna vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama milioni 2.2 na mtaji wa shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya wanachama wa VICOBA ni wanawake,” amesema.
Amezitaka Halmashauri zote nchini ziweke orodha sahihi ya vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa vilivyosajiliwa kwa kila kijiji na kuchukua hatua za kuwezesha uanzishaji na usajili wa SACCOs zinazokidhi vigezo kulingana na shughuli za uzalishaji katika Halmashauri husika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, APRILI 22, 2016.