Home » Tanzania » Ukaguzi wa magari madogo kuanza Machi mosi

Ukaguzi wa magari madogo kuanza Machi mosi

23 February 2018 | Tanzania
Na Leandra Gabriel, Globu ya Jamii.
BARAZA la Taifa la usalama barabarani  limetangaza kuanza kwa ukaguzi wa magari madogo ya binafsi nchini nzima kuanzia Machi moja mwaka huu, huku likieleza kuwa linatafuta mfadhili atakayesaidia kufunga kamera kwenye baadhi ya makutano ya barabara ili kuwakamata bodaboda watakaofanya makosa.
 
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es saalam na mwenyekiti wa baraza hilo Mhandisi Hamad Masauni ambaye pia ni Naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi wakati akielezea tathimini ya utekelezaji wa  mpango mkakati wa kudhibiti ajali za barabarani ambapo inaonesha ajali zimepungua. Akizungumzia kuhusu waendesha bodaboda amesema, baadhi yao wamekuwa wakikiuka sheria za usalama barabarani kwa kufanya makosa mbalimbali na baadhi ya makosa hayo ni kupita katika taa nyekundu, kutovaa kofia ngumu na kubeba abiria zaidi ya mmoja.
 
Hivyo amesema baraza limepanga kutoa elimu maalumu itakayosaidia kupunguza ajali na kuhakikisha wanaovunja sheria wanachukuliwa hatua.“Hatua hizo zitasaidia kuwajengea uelewa wa usalama barabarani watumiaji wa barabara na madereva wataogopa kufanya makosa barabarani na hivyo na kuwa na utii wa sheria bila shuruti.”
 
Pia amesema wamebaini kuwa, pikipiki nyingi zimesajiliwa kwa majina ya kampuni zinazouza pikipiki badala ya majina ya wamiliki wa pikipiki hizo kitendo ambacho ni kinyume na sheria na kimekua kikisababisha usumbufu katika ukamataji wa bodaboda.Hivyo, Masauni amesema pikipiki ambazo zitakamatwa na kubainika zimesajiliwa kwa majina ya kampuni badala ya jina la mmiliki wenye kampuni hizo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
 
Kuhusu wa magari madogo, Masauni amesema awamu ya pili ya mpango mkakati wa kupunguza ajali za barabarani wamefanikiwa kukagua magari makubwa, magari ya abiria, magari ya mizigo na magari yanayobeba wanafunzi ambapo wamefanikiwa kufanya ukaguzi huo kwa asilimia 79.
 
Amesema hivyo awamu ya tatu ni kwa magari madogo ambapo amehimiza wenye magari kufanya ukaguzi huo ambao utafanyika kwa kipindi cha miezi miwili na baada ya hapo ambao watakabainika kutokuwa na stika zinazoonesha kutokaguliwa kwa magari yao watachukuliwa hatua.
 
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani , Fortunas Musilimu amesema kuwa watu wote wenye magari kuhakikisha magari yao yanakaguliwa katika maeneo maalumu na kueleza wamekuwa makini kwa kuhakikisha gari inayobandikwa stika ni ile ambayo itakuwa imekaguliwa na si vinginevyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari(hawapo pichani), ambapo alitangaza kuanza rasmi kwa zoezi la ukaguzi wa magari binafsi mwanzoni mwa mwezi ujao.Wengine ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, SACP Fortunatus Musilimu na Mjumbe wa baraza hilo,Henry Bantu(kushoto).Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa wizara, jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, SACP Fortunatus Musilimu, akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), ambapo ilitangazwa operesheni ya ukaguzi wa magari binafsi unaotarajiwa kuanza mwezi machi mwanzoni.Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni, Mkutano huo umefanyika leo latika ukumbi wa wizara, jijini Dar es Salaam. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Henry Bantu, akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), ambapo ilitangazwa operesheni ya ukaguzi wa magari binafsi unaotarajiwa kuanza mwezi machi mwanzoni.Katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini,Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, SACP Fortunatus Musilimu(kulia). Mkutano huo umefanyika leo latika ukumbi wa wizara, jijini Dar es Salaam. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA),Geoffrey Silanda, akijibu baadhi ya maswali yaliyoelekezwa kwake wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari(hawapo pichani).Mkutano huo umefanyika leo latika ukumbi wa wizara, jijini Dar es Salaam. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Ad