Home » Tanzania » Serikali Yatoa Ripoti Mwenendo wa Kipindupindu Nchini

Serikali Yatoa Ripoti Mwenendo wa Kipindupindu Nchini

19 January 2016 | Tanzania

SERIKALI kupitia Wizara ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto leo imetoa ripoti yake ya wiki juu ya mwenendo wa kipindupindu hapa nchini.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam katika ofisi za wazara hiyo, Mkurugenzi wa Huduna za Kinga Nchini, Dk. Neema Rusibamayila amesema kuwa katika kipindi cha wiki moja kuanzia Januari 11 hadi 17,2016 kulikuwa na wagonjwa wapya 549 na vifo 10 huku mikoa iliyoripoti kuwa na ugonjwa ikiongezeka kutoka 11 hadi kufikia 16 ukilinganisha na wiki iliyopita.

Rusibamayila amesema, mikoa hiyo iliyoongezeka kwa kurudia kuripoti wagonjwa wapya baada ya kudhibiti ugonjwa kwa wiki zilizopita ni Dar es Salaam, Lindi, Rukwa, Kagera na Kilimanjaro huku akiongeza kuwa bado kuna mikoa inaendelea kuripoti wagonjwa ikiwa ni pamoja na Morogoro, Arusha, Singida, Manyara, Pwani ,Dodoma, Geita, Mara, Tanga, Mwanza na Simiyu.

Aidha, alisema Mkoa wa Morogoro unaendelea kuripoti idadi kubwa ya wagonjwa (Manispaa ya Morogoro wagonjwa 120, Halmashauri ya Morogoro wagonjwa 40 ) ikifuatiwa na Mkoa wa Simiyu wenye idadi ya watu 50.

Hata hivyo, Rusibamayila ameeleza namna mwananchi anavyoweza kupata huduma ya kufahamu dalili za ugonjwa huo wa kipindupindu kupitia njia ya simu ya mkononi kwa kupiga namba 117 kisha  kusikiliza ujumbe wa sauti, au kuandika ujumbe wa maneno “kipindupindu/cholera” kwenda namba 15774  na huduma hiyo haina malipo yoyote kwa mtumiaji.

Alisema kuanzia Agosti mwaka jana ugonjwa huo ulipoanza hapa nchini hadi jana Januari 17, 2016  jumla ya watu 14,105 wameugua ugomjwa huo na kati yao 218 wamepoteza maisha kwa maradhi hayo ya kipindupindu.

Ad