Rais Magufuli aongoza mapokezi ya ndege ya pili aina ya Airbus A220-300
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Januari, 2019 ameongoza mapokezi ya ndege mpya aina ya Airbus A220-300 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ndege hiyo ni ya pili ya aina ya Airbus 220-300 kununuliwa na Serikali kwa ajili ya ATCL na ni ndege ya 6 kuwasili hapa nchini kati ya ndege 7 ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imezinunua kwa lengo la kuimarisha usafiri wa anga, kukuza utalii, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
Sherehe za mapokezi ya ndege hiyo zimefanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal One) Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O’donnel, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge, viongozi wa Dini, viongozi wa siasa, wafanyabiashara, viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.
Akizungumza baada ya kuipokea na kuizindua ndege hiyo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania wote kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake ikiwemo kununua ndege 7 zilizowezesha kuimarishwa kwa ATCL pamoja kutekelezwa kwa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) na mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji, na kwamba kwa mwendo huu mambo mengine mengi makubwa yanakuja.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi na wafanyakazi wote wa ATCL kwa kazi nzuri wanayofanya wakiwemo Marubani vijana wa Kitanzania watatu walioendesha ndege hiyo kutoka Montreal nchini Canada hadi Jijini Dar es Salaam Tanzania, na amebainisha kuwa hayo ni matunda ya kununua ndege mpya na kuimarisha ATCL.
“Tumeambiwa hapa tangu tuanze kununua ndege hizi ATCL imeongeza idadi ya Marubani kutoka 11 hadi 50, walioajiriwa ni vijana wetu wa Kitanzania, na kwa ujumla wafanyakazi wapya wa ATCL walioajiriwa ni 380, hivi kama tusingenunua ndege hizi vijana hawa wangeendesha nini? Wangeendesha matoroli? Lakini sasa wamepata ajira wananufaika wao na familia zao au jamaa zao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa ndege hizi zote zimenunuliwa kwa fedha za Watanzania kwa asilimia 100, na amewataka Watanzania wote kuelewa kuwa maendeleo ya Tanzania yataletwa na Watanzania wenyewe na kwamba hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea kwa kutegemea misaada.
“Tunahitaji misaada lakini iwe ni misaada ya kutuwezesha kusonga mbele kimaendeleo na kujitegemea na sio kutulemaza, sekta binafsi pia tunaihitaji lakini iwe ni sekta binafsi ya manufaa kwa Taifa.
Hata leo amekuja mwenyekiti wa Bharti Airtel, tumezungumza na amekubali kuongeza hisa za Serikali katika airtel kutoka 40 hadi 49 na kupunguza hisa kwenye kampuni yake kutoka asilimia 60 hadi 51 bila kutudai malipo yoyote, pia Airtel itatoa gawio kwa Serikali wakati miaka minane yote ya nyuma haikuwahi kutoa hata senti tano” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza ndege mbili za Serikali (Fokker 28 na Fokker 50) zilizokuwa zikitumiwa kusafirisha viongozi zipigwe rangi za ATCL na kuanza kusafirisha abiria ili kuiongezea uwezo ATCL na kuwawezesha Watanzania wote kupata huduma za usafiri wa anga.
Mapema Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson ameipongeza Serikali kwa juhudi kubwa za kuimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege mpya, na amefafanua kuwa anafurahi kuona matunda ya fedha zinazopitishwa na Bunge katika bajeti.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuongoza juhudi za kuleta mageuzi ya kiuchumi hapa nchini na amemhakikishia kuwa Watanzania wanamuunga mkono na wapo tayari kuhakikisha nchi yao inasonga mbele.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Januari, 2019