Rais Magufuli akutana na mabalozi wa Canada na Aljeria na aagana na Balozi wa Vatican
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameikaribisha nchi ya Canada kushirikiana na serikali yake ya awamu ya tano katika kuleta mageuzi ya kiuchumi, hususani katika uwekezaji kwenye sekta ya Kilimo, Madini, Uvuvi na Huduma za kijamii.
Rais Magufuli ametoa ujumbe huo alipokuwa akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini Mheshimiwa Alexandre Le've'que aliyekutana nae Ikulu Jijini Dar es salaam na kupokea barua yenye ujumbe wa Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa Justin Trudeau.
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amesema serikali yake hairidhishwi na jinsi kilimo cha Tanzania kisivyowanufaisha wakulima ipasavyo, na hivyo ameikaribisha nchi ya Canada hususani sekta binafsi ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na uvuvi ili kuzalisha ajira na kuongeza thamani ya mazao kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Dkt. Magufuli pia ametaka Canada yenye uwezo mkubwa kiteknolojia na mtaji ishirikiane na Tanzania katika uwekezaji kwenye sekta ya madini na gesi kwa kujenga viwanda vya kuchakata madini ndani ya nchi ya Tanzania na pia rasilimali ya gesi ambayo mpaka sasa Tanzania imethibitika kuwa na hifadhi ya futi za ujazo zaidi ya Trilioni 57.
"Mheshimiwa Balozi Alexandre Le've'que naomba ukamweleze Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa Justin Trudeau kuwa Tanzania na Canada sio tu ni nchi marafiki bali pia ni ndugu wenye uhusiano wa kihistoria. Ningependa kuona Canada inashirikiana na serikali yangu, katika juhudi zake za kuachana na usafirishaji wa mchanga wa madini badala ya madini yaliyochakatwa na pia kuachana na usafirishaji wa mazao yakiwa ghafi" Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Balozi wa Canada hapa nchini Mheshimiwa Alexandre Le've'que amemhakikishia Rais Magufuli kuwa atafikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu Canada Mheshimiwa Justin Trudeau, na amebainisha kuwa nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika juhudi zake za kuimarisha uchumi, hasa baada ya kujionea juhudi za Rais Magufuli katika kukabiliana na rushwa, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kusimamia nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Aljeria Mheshimiwa Abdelaziz Bouteflika ambaye pamoja na kumpongeza kwa hatua anazochukua katika uendeshaji wa serikali, amemhakikishia kuwa Aljeria ipo tayari kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania huku akitaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni nishati na kilimo.
Ujumbe wa Rais Bouteflika umewasilishwa kwa Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam na Balozi wa Aljeria hapa nchini Mheshimiwa Belabed Saada.
Rais Magufuli amemhakikishia Rais Bouteflika kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Aljeria, na kwamba hivi karibuni imepanga kuanzisha ofisi za Ubalozi katika nchi hiyo.
Kuhusu sekta za nishati na kilimo, Rais Magufuli amesema serikali yake inakaribisha uwekezaji kutoka Aljeria hasa wakati huu ambapo Tanzania imethibitika kuwa na kiasi kikubwa cha gesi, na kwa upande wa kilimo ametoa wito kwa Aljeria kushirikiana na Tanzania katika mpango wake wa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, ikiwemo usindikaji wa zabibu, viwanda vya nguo, viwanda vya ngozi na nyama na viwanda vya kusindika minofu ya samaki.
"Naomba ukamweleze Mheshimiwa Rais Bouteflika kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Aljeria na kwamba imefurahishwa sana kuona Aljeria ipo tayari kusaidia juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo nchini Tanzania" Rais Magufuli amemweleza Balozi Belabed Saada.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na Balozi wa Vatican hapa nchini Mheshimiwa Francisco Montecillo ambaye anamaliza muda wake baada ya kuiwakilisha Vatican kwa muda wa miaka minne na nusu.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
22 Aprili, 2016