Rais Magufuli aagiza walioficha sukari waifichue mara moja
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wafanyabiashara wote walioficha sukari katika maghala yao, kuanza kuisambaza mara moja, vinginevyo serikali itachukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuinyang'anya sukari hiyo na kuisambaza kwa wananchi bure.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 06 Mei, 2016 katika mikoa ya Singida na Manyara wakati akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti waliosimamisha msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kwenda Arusha.
Dkt. Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuwafuatilia wafanyabiashara wanaofanya njama za kuficha sukari na kusababisha upungufu wa bidhaa hiyo, na ameapa kuwa serikali yake itawachukulia hatua kali watakaobainika kufanya hivyo.
Pamoja na kutoa maagizo hayo Rais Magufuli amewaondoa shaka watanzania juu ya upungufu wa sukari, kuwa serikali imeagiza sukari kutoka nje ya nchi ambayo itasambazwa kwa wananchi kwa bei nafuu ili kufidia upungufu uliopo.
"Wale wote waliokuwa wameficha sukari waiachie, wasipoiachia sukari, huwezi kuificha kama sindano, nimeshaagiza vyombo vya dola, vikague magodown yote, atakayekutwa na sukari ameificha, yule ni mhujumu uchumi kama wahujumu wengine, asije akanilaumu, asijee-akanilaumu, na ninasema kwa dhati, wewe mfanyabiashara uliyepata nafasi ya Tanzania kuleta bidha za sukari, halafu unanunua unakwenda kuficha ili kusudi wazee hawa wahangaike, ili mwezi mtukufu wa Ramadhani utakapoingia watu wakose sukari, dawa yao ninayo" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, akizungumza katika miji ya Katesh, Babati, Dareda na Magugu Mkoani Manyara Dkt. Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kukosa maeneo ya kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji, na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Joel Bendera na wakuu wilaya za mkoa huo kukamilisha mchakato wa kuyapitia mashamba yote yaliyotelekezwa na wamiliki wake, kisha wawasilishe taarifa kwake ili afute hati za umiliki wa mashamba hayo na kuamuru wagawiwe wananchi.
"Kero kubwa katika maeneo haya, pamekuwa na mashamba makubwa ambayo yalichukuliwa na wenye pesa, halafu yale mashamba hawayaendelezi, na wanapoacha kuyaendeleza wanawachukua wananchi masikini na kuanza kuwakodisha, kwa kukusanya fedha, mniachie hili ndugu zangu nitalishughulikia" Amesisitiza Dkt. Magufuli.
Mjini Babati Rais Magufuli amepokea kilio cha wananchi waliodai kudhulumiwa haki zao na kujikuta wakipoteza mali ikiwemo nyumba za kuishi na mazao na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupanga siku za kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Rais Magufuli amewasili Mjini Arusha akitokea Dodoma kwa njia ya barabara na kesho anatarajia kutunuku kamisheni kwa maafisa wapya wa Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 58/15 katika chuo cha mafunzo ya jeshi Monduli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
06 Mei, 2016