Home » Tanzania » Rais Dr. Magufuli amlilia Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi

Rais Dr. Magufuli amlilia Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi

15 August 2016 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea leo tarehe 14 Agosti, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Mwaka 1972 hadi 1984.

Kufuatia kifo hicho Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alijitoa kupigania Uhuru, Umoja, Haki na Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilikipitia.

"Nimeshitushwa sana na kifo cha Mzee wetu Mhe. Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake alitoa mchango mkubwa wa kuipigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo" Amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli ameendelea "Kupitia kwako Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein napenda kuwapa pole familia ya Marehemu, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote, Wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla kwa kufikwa na msiba huu mkubwa"

Rais Magufuli amemuombea marehemu Aboud Jumbe Mwinyi apumzike mahali pema peponi.

.

 

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es Salaam

14 Agosti, 2016

 

Ad