Home » Tanzania » Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini waelekea kamilika

Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini waelekea kamilika

01 March 2016 | Tanzania

Huduma ya Usambazaji wa Maji Safi katika jiji la Dar es salaam inatarajiwa kuimarika kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi. Ujenzi wa Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.

Mradi huo unajengwa na Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure kwa gharama ya shilingi Bilioni 141 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania na una  jumla ya urefu wa kilometa 55.9.

Akizungumzia mradi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa , Romanus Mwang’ingo amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa bomba hilo kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam

 Amesema ujenzi wa mradi huo kutoka mtambo wa Ruvu Chini ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani na kuongeza kuwa utakapokamilika utazalisha lita milioni 270 kwa siku kutoka lita milioni 182 ambazo zote zitasukumwa kuja jijini Dar es salaam.
 

 Aidha, amesema kasi ya mkandarasi ya kulaza bomba hilo inaridhisha licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazochelewesha kazi hiyo zikiwemo za ufinyu wa eneo linapojengwa bomba hilo kuwezesha mitambo kufanya kazi vizuri katika eneo la mbezi Beach, mvua zinazoendelea kunyesha ,changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 Mahakamani zikihusisha madai mbalimbali ya wananchi katika maeneo hayo.

“Ni kweli zipo changamoto zilizosababisha mradi kukawia kumalizika zikiwemo za wananchi kufungua kesi 17  Mahakama ya Ardhi, hadi sasa DAWASA tumeshinda kesi 14  ndiyo maana tumepata haki ya kutumia njia hii kukamilisha upanuzi wa mradi” Amesema Mwang’ingo.

Ameongeza kuwa lengo la mradi huu nikuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha huduma kwa wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani.

Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, Kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo na Vingunguti.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kampuni inajenga bomba hilo nchini Muhandisi Eric Omuruli akizungumzia mradi huo amesema kuwa yeye kama Meneja mradi atahakikisha anashughulikia changamoto zilizopo ili kukamilisha kwa wakati.

Ad