Home » Tanzania » Rais Magufuli apongeza Mkapa Foundation na Global Fund

Rais Magufuli apongeza Mkapa Foundation na Global Fund

11 July 2017 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Taasisi ya Mkapa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa mchango wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi zikiwemo kujenga zahanati, nyumba za watumishi wa afya na shule.

Mhe. Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 10 Julai, 2017 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Chato Mkoani Geita muda mfupi baada ya Msarifu wa Taasisi ya Mkapa ambaye ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kukabidhi nyumba 50 za watumishi wa afya kwa Mikoa ya Geita, Kagera na Simiyu zilizojengwa na taasisi hiyo.

Mhe. Dkt. Magufuli ametoa wito kwa taasisi nyingine zilizopo hapa nchini kuiga mfano mzuri uliooneshwa na Taasisi ya Mkapa kwa kufanya kazi zenye manufaa kwa wananchi na Taifa badala ya kuhamasisha mambo yasiyo na manufaa.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha huduma za Afya hapa nchini ikiwemo kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ametoa wito kwa wakurugenzi na watendaji wote wanaosimamia fedha hizo kuzitumia vizuri.

“Viongozi wetu wa halmashauri wa wilaya na mikoa msimamie miradi yetu kikamilifu, Watanzania hawa wana matumaini makubwa na Serikali yao, wamechoka kuonewa kila siku, na ndio maana nazungumza kila siku Serikali ninayoiongoza itakuwa upande wa wananchi, hasa wananchi wanyonge” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Pia Mhe. Rais Magufuli ameonya dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma unaofanywa katika miradi na huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali huku akibanisha kuwa Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa pembejeo za ruzuku ambapo mpaka sasa katika mikoa 11 iliyowasilisha madai ya Shilingi Bilioni 50 imebainika kuwa madai halali ni Shilingi Bilioni 8.

Kwa upande wake Msarifu wa Taasisi ya Mkapa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha huduma za afya na amesema taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kuimarisha huduma za afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakichangia gharama za kuboresha huduma hizo.

Mapema akitoa taarifa ya Taasisi ya Mkapa, Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Dkt. Ellen Mkondya Senkoro amesema kati ya nyumba 50 zilizokabidhiwa leo, 20 zimejengwa Geita, 20 zimejengwa Simiyu na 10 zimejengwa Kagera na kwamba nyumba hizo ni kati ya nyumba zote 450 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 26.5 zilizojengwa na taasisi hiyo tangu mpango ulipoanzishwa mwaka 2012.

Dkt. Senkoro ameongeza kuwa pamoja na kujenga nyumba hizo, Taasisi ya Mkapa imeajiri watumishi wa afya 1,100 na imejenga vituo 11 vya afya vinavyotoa huduma ya upasuaji nchini.

Nae Mwakilishi wa Mfuko wa Dunia (Global Fund) Bi. Matha Setembo  amesema tangu mwaka 2003 hadi 2017 mfuko huo umeingia mikataba Serikali ya Tanzania yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.8 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria na kwamba kati ya mwaka 2018 – 2020 Mfuko huo umetenga takribani Shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya Tanzania Bara na takribani Shilingi Bilioni 24.5 kwa ajili ya Zanzibar ili kukabiliana na magonjwa hayo.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida ambaye amekabidhi kiwanda cha alizeti kwa chama cha ushirika cha msingi Chato, ameahidi kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ambaye amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa kipaumbele kwenye huduma za afya ikiwemo kuongeza fedha za dawa na hivyo kuwezesha bei ya dawa katika vituo vya tiba kupungua kwa kati ya asilimia 15 na asilimia 80.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato, Geita

10 Julai, 2017

 

Ad