Rais Dkt. John Pombe Magufuli mgeni rasmi sherehe za mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania
Serikali itaendelea kusimamia ubora wa elimu kwa kuhakikisha shule na taasisi zinadahili wanafunzi wenye sifa stahiki za kujiunga na kozi wanazoomba.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa kauli hiyo katika sherehe za mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania zilizofanyika Bungo, Kibaha Mkoani Pwani.
Kabla ya Rais Magufuli kutoa kauli hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Prof. Elifas Tozo Bisanda alieleza kuwa chuo hicho kimeshindwa kudahili idadi kubwa ya wanafunzi baada ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuzuia udahili wa wanafunzi wanaotaka kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwa kutumia sifa ya kupatiwa kozi ya awali (Foundation Course) ambayo imekuwa ikitumiwa na wanafunzi wasio na sifa za kujiunga vyuo vikuu kwa vigezo vya TCU.
"Kwa vile mnachukuliwa sawa na vyuo vingine ni lazima mzingatie vigezo vya mtu kuitwa mhitimu wa Chuo Kikuu, kwa hiyo nasema kwa dhati nakubaliana sana tena kwa asilimia 100 na yale yaliyozungumzwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako.
"Kwa hiyo ni lazima hili suala la kuweka viwango vya ubora wa elimu yetu tulizingatie, ni mara kumi tuwe na wanafunzi hata 10 wanaohitimu elimu ya juu kuliko kuwa na wanafunzi 20,000 wakati hawana sifa, kwa sababu tutakapokwenda kwenye ajira hatutauliza kama huyu ametoka Chuo Kikuu Huria, huyu ametoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ama huyu ametoka Chuo Kikuu cha Dodoma, wote tutawaangalia kwa usawa.
"Tusitafute njia ya mkato, njia ya mkato ni mbaya, kwa hiyo kwa hili kwa kweli Mhe. Prof. Ndalichako nakubaliana na wewe, nafikiri ndio maana umekuwa Waziri wa Elimu, tunataka kulinda hadhi ya elimu yetu" amesema Dkt. Magufuli.
Hata hivyo, Rais Magufuli amekipongeza Chuo Kikuu Huria kwa kazi nzuri ya kutoa elimu ya juu kwa Watanzania wengi na kuanzisha matawi katika nchi mbalimbali za Afrika na ameahidi kuwa Serikali yake itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto za miundombinu na mahitaji mengine.
Aidha, Rais Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za Serikali ambao wamekuwa wakitumia vibaya fedha za umma ikiwemo kuweka fedha nyingi za Serikali katika akaunti za muda maalum (Fixed Deposit Account) kwenye benki za biashara ambako hujipatia fedha kupitia faida ya akiba bila kujali kuwa vitendo hivyo husababisha Serikali kukosa fedha na kulazimika kukopa kutoka benki za biashara ambako hutozwa riba kubwa.
"Sasa sifahamu kama Chuo Kikuu Huria na nyinyi mmekuwa mkiweka fedha za maendeleo katika Fixed Deposit Account, lakini huo ndio umekuwa ni mchezo, juzi hapa tumekuta fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 26 zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye benki tatu kama Fixed Deposit Account na Bodi ya TRA ikapitisha, ndio maana nilipozipata hizo taarifa, fedha nikachukua na Bodi kwa heri.
"Hata kwa sasa hivi Waziri upo hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ilianzishwa kwa sababu maalum, inachangiwa fedha wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye Fixed Deposit Account, Waziri hiyo ni message sent and Delivered" amesisitiza Rais Magufuli.
Katika Mahafali hayo, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amewatunuku shahada na vyeti jumla ya wahitimu 4038, wakiwemo wahitimu 8 wa shahada ya Uzamivu, 217 wa shahada ya Uzamili, 111 wa Stashahada ya Uzamili, 1,186 wa Shahada ya Kwanza, 484 wa Stashahada na 1,421 wa vyeti mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Novemba, 2016