Home » Afrika » Rais wa Zambia Edga Lungu ameapishwa

Rais wa Zambia Edga Lungu ameapishwa

14 September 2016 | Afrika

Rais wa Zambia Edga Lungu ameapishwa hii leo baada ya kuchaguliwa tena wakati wa uchaguzi wa mwezi Agosti.

Kuapishwa kwake kunafanyika baada ya upinzani kushindwa katika kesi ya kutaka matokeo ya uchaguzi kubatilishwa.

Mahakama ya katiba ilitupilia mbali kesi ikisema kuwa upinzai ulikuwa umeishiwa muda wa kupeleka suala hilo mahakamani.

Bwana Lungu alishinda uchaguzi wa tarehe 11 mwezi Agosti kwa asilimia 50.35 na kupita kiwango kilichokwa kuepuka kurudiwa tena kwa uchaguzi.

Hakainde Hichilema ambaye alichukua nafasi ya pili kwa asilimia 47.63 anaendelea kupinga matokeo hayo.

Kuelekea kuapishwa kwa rais Lungu, Hichilema alikwenda Mahakamani kupinga ushindi wake lakini Mahakama ya Kikatiba ikatupilia mbali kesi yake.

Hichilema ambaye amewania urais mara tano bila mafanikio, amesema sherehe za kumwapisha rais Lungu hazikuwa halali na zimekwenda kinyume na Katiba ya Zambia.

“Mahakama haikutoa uamuzi kuwa rais Lungu alishinda uchaguzi huu. Huu ni uvunjifu wa Katiba. Ukweli ni kwamba kura zetu ziliibiwa,” alisema Hichilema.

Viongozi kadhaa wa bara Afrika walihudhuria sherehe hizo zilizofanyaika jijini Lusaka akiwemo rais wa Zimbabwe Robert Mugabe.

Takribani watu 60,000 wamehudhuria kuapishwa kwa Rais huyo.

Ad