Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na Mkapa ,Jaji Warioba
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Januari, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba Ikulu Jijini Dar es salaam.
Akizungumza mara baada ya Mazungumzo hayo Rais Mstaafu Mkapa amesema lengo la kukutana na Rais Magufuli ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na watanzania kuiongoza nchi, kuunda serikali na kumtakia heri ya Mwaka Mpya.
Rais Mstaafu Mkapa pia amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba pamoja na kumtakia heri ya Mwaka Mpya, amempongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri hususani katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu ambayo yanawahusu wananchi yakiwemo afya na maji.
Jaji Warioba ameongeza kuwa Watanzania wote wanapaswa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi kubwa anazofanya, ambazo ni kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali ya umma.
"Lazima kila mmoja amuunge mkono Rais, tusije tukamuachie, pale ulipo kama ni mambo ya rushwa uanzie hapo hapo, kama ni mambo ya matumizi mabaya ya madaraka anzia hapohapo, tusije tukamuachia Rais pekee yake, yeye awe kiongozi wetu, lakini watanzania wote tushughulike na matatizo hayo" alisisitiza Jaji Warioba.
Gerson Msigwa,Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULUDar es salaam07 Januari, 2016