Home » Makala » Watafiti wamulike huku

Watafiti wamulike huku

27 April 2016 | Makala

Najua unaweza ukashtuka lakini hautakiwi kupepesuka kwani umefika wakati kwa Wananchi kuweza kuambiwa ukweli dhidi ya Viongozi wao, kuambiwa ukweli dhidi ya matendo na hali za viongozi wao zilivyo kabla na baada ya kuingia madarakani.

Kwa wale wenye kumbukumbu sawia watakumbuka kuwa mwishoni mwa Mwaka jana zilitolewa tafiti mbalimbali za hali za kiuchumi za Wanasiasa na Wafanyabiashara. Mathalani tulipashwa kuwa Mnigeria Aliko Dangote ndiye kinara wa utajiri Afrika.

Jarida la Forbes limemweka kama mtu wa 51 kwa utajiri duniani akiwa na hazina ya utajiri unaofikia dola bilioni 15.4 . Utajiri wake ni mara mbili ya mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich ambaye anashika nafasi ya 137 Duniani.

Dangote alizaliwa kwenye familia ya wafanyabiashara katika jiji la Kano ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini Nigeria. Akiwa na umri wa miaka 21, mjomba wake akampa mkopo wa kuanzisha biashara yake mwenyewe.

Bwana Dangote ameorodheshwa tajiri wa 51 Duniani ukilinganisha na nafasi ya 67 mwaka 2015 wakati gazeti hilo la Forbes lilipoiweka mali yake kufikia dola bilioni 14.7.

Hali kadhalika tuliambiwa nchi za Afrika Mashariki nazo zina mbabe wake mwenye nguvu kubwa kiuchumi. Ndiye anayeongoza katika `ligi’ ya utajiri wa fedha kwa nchi kadhaa za Kusini mwa Jangwa la Sahara, zikiwemo Tanzania, Uganda na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Msumbuji na hata Zambia.

Jarida maarufu la Forbes linamtaja mbabe huyo kuwa ni Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Kenya. Uhuru anatajwa kuwa ndiye mtu tajiri zaidi kuliko wote katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Kwa Afrika, Uhuru anashika nafasi ya 26, lakini kwa Kenya na Afrika Mashariki, ndiye kinara kutokana na kuwa na utajiri unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 600 (Sh bilioni 995 za Tanzania). Uhuru Kenyatta ni mmoja wa watu wawili tu wa Afrika Mashariki waliomo orodha ya mabilionea 40 wanaotambuliwa barani Afrika.

Mwingine, Chris Kirubi pia raia wa Kenya, ndiye anayeshika nafasi ya pili kwa utajiri Afrika Mashariki, wakati barani Afrika anashika nafasi ya 31. Akiwa na umri wa miaka 70, amefanikiwa kukusanya utajiri wa dola milioni 300, sawa na Sh bilioni 480 za Tanzania! 

Uhuru, mtoto wa kwanza wa Jomo Kenyatta, ana utitiri wa biashara na ardhi ya kutosha ndani ya Kenya. Anatajwa kuwa na zaidi ya ekari 500,000 ndani ya Kenya, akirithi ardhi iliyotwaliwa na baba yake katika miaka ya 1960 na 1970.

Anamiliki kiwanda kikubwa cha bidhaa za maziwa cha Brookside Dairies, kituo maarufu cha televisheni cha K24, benki na hisa katika moja ya mashirika makubwa ya ndege nchini humo, achilia mbali biashara nyingine kubwakubwa za ndani na nje ya Kenya.

Wakati Wakenya hao wakichomoza katika orodha ya matajiri 40 wa Afrika, Tanzania haina hata bilionea mmoja.

Kama hiyo haitoshi, pia tulisikia kutajwa kwa Wafanyabiashara Said Salim Bakhressa, Gulam Dewji, Rostam Aziz, Reginald Mengi, Mohammed Dewji na Ali Mufuruki, wakitajwa na Jarida la Ventures Africa linalozungumzia masuala mbalimbali ya uchumi wa Afrika kuwa ndiyo matajiri zaidi nchini.

Kwa mujibu wa gazeti lilieleza vizuri kuwa “anayeongoza katika orodha hiyo ni Bakhressa anayemiliki mali na fedha zenye thamani ya Dola za Marekani 620 milioni sawa na Sh992 bilioni (Dola moja Sh1,600) akifuatiwa na Dewji ambaye utajiri wake ni Dola 560 milioni (Sh896 bilioni).

Wengine na kiasi cha mali na fedha wanazomiliki kwenye mabano ni Rostam (Sh672 bilioni- Dola 420 milioni) Mengi (Sh448bilioni- Dola 280 milioni) na Mufuruki (Sh176 bilioni - Dola 110 milioni).

Kwa upande wa Said Salim Bakhresa Jarida hilo lilisema chanzo cha utajiri wa Bakhressa ni mapato yanayotokanana uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenye viwanda vyake.

Mfanyabiashara huyo aliacha shule akiwa na umri wa miaka 14 na kuanzisha biashara zake. Alianza kuuza urojo Zanzibar na baadaye alifungua mgahawa miaka ya 1970.

Mgahawa huo ulipanuka na alitumia faida yake kufungua mashine ya kusaga pamoja kiwanda za usindikaji vyakula, huku akiunda Kundi la Makampuni ya Bakhressa.

Aliendelea kusindika vyakula mbalimbali na kutengeneza unga wa mahindi na baadaye kuanzisha kiwanda cha kuoka mikate na baadaye kutengeneza chocolate, ice cream, vinywaji na makasha ya kufungashia bidhaa. Kutokana na shughuli hizo, kwa mwaka huingiza Sh800 milioni.

Kampuni zake kwa sasa zinafanya biashara mbalimbail katika nchi za Tanzania, Uganda, Malawi, Rwanda na Msumbiji na ameajiri zaidi ya wafanyakazi 2,000”.

Katika ripoti za tafiti zote hatujawahi kusikia kutajwa kwa Viongozi wetu kuwamo katika makundi tajwa. Je, ni kweli viongozi wetu tulionao ni maskini? Hawana utajiri wowote ule jamii unaoufahamu? Je, maskini kama sisi tusiokuwa na madaraka? Je, ni maskini kama sie tusio na ilani ya kuizungumzia?

Wakati nikiyawaza hayo nikapata wazo la kutokuanzia mbali juu ya kufikiri dhidi ya viongozi wetu ambapo jina la haraka haraka lililokatiza fikrani ni la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli almaarufu kama JPM ambaye kwa sasa ndiye “top” wa kimadaraka (ni Rais) na ndiye amepewa Ilani ya Uchaguzi aitekeleze huku tukishuhudia serikali yake ikitenga Mabilioni ya mapesa kufanikisha zoezi zima la utekelezaji wa ilani hiyo.

Kwa wale Wanaomfahamu JPM hana historia ndefu wala hana historia fupi ya Kiungozi lakini mafanikio aliyoyapata kipindi kifupi ni makubwa kuliko historia ya maisha yake ya kisiasa. Hilo halina ubishi.

Hapa panahitajika utulivu na umakini mkubwa ili tupate kuyang’amua mafanikio aliyoyavuna Rais Magufuli ndani ya kipindi kifupi kabisa cha maisha yake ya kisiasa yatakayomfanya aingie kwenye orodha ya viongozi watakaokumbukwa na Wananchi kutokana na utajiri wa aina yake alionao.

Kwa upande wa pili ningependa tuyamulike maeneo machache sana ambayo yamemjengea utajiri mkubwa sana Rais Magufuli ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake akiwa kama Rais wa nchi.

Hivi karibuni tumemsikia Mkaguzi mkuu wa mahesabu ya Serikali CAG Profesa Asad akiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa mwaka 2014/15 ambapo imeonyesha zaidi ya bilioni 300 zimetafunwa na wajanja huku kiasi kikubwa kikiliwa kwenye semina, posho na safari za nje hali iliyopelekea mpaka taasisi nyeti kupewa hati chafu.

Rais Magufuli ambaye alishawahi kuwa Waziri kwa miaka 20 mfululizo anajua madudu mengi ya Serikali aliamua kulivalia njuga suala la matumizi mabaya ya pesa za Serikali kwa kufutilia mbali semina, kulipana posho na safari za nje zisizo na tija kwa watumishi wa umma na anayetaka kusafiri ni lazima apate kibali maalum cha serikali na hivyo kufanikiwa vilivyo kubana matumizi ya Serikali na pesa zote zinazookolewa zitapelekwa kwenye matumizi ya matumizi.

Hapa Rais Magufuli aliwakuna kweli Watanzania waliochoshwa kuona anasa za watumishi wa umma huku wao wakiishi maisha magumu ya hata kushindwa kupata mlo mmoja.

Katika kuonyesha anayaishi maneno yake hata yeye mwenyewe amejizuia kusafiri safari ovyo ovyo nje ya nje kama ambavyo tulizoea kuona viongozi wakuu wakipishana angani utadhani nchini kunawaka moto.

Tangu aingie madaraka Rais Magufuri amesafiri safari moja tu ya nje ya nchi ya kwenda nchini Rwanda nchi jirani na Tanzania. Kitendo hichi cha kutokusafiri nje ya nchi kumeokoa mabilioni ya pesa ambazo zitatumika kwa matumizi ya kimaendeleo.

Rais Magufuli amekabidhiwa nchi ikiwa na uwezo wa makusanyo ya ndani ya Tsh. bilioni 800 tu toka kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete lakini ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tu alifanikiwa kupata makusanyo ya ndani ya mapato yetu hadi kufikia Trilioni moja kwa mwezi na hivyo kuonyesha mwanga mzuri wa kupunguza hali ya utegemezi toka nje.

Mpaka sasa Serikali inakusanya trilioni 1.5 kwa kila mwezi hali iliyopelekea kutoa pesa nyingi kwenye shughuli za kimaendeleo kwani uwezo unaruhusu. Nani kama Magufuli?

Ni Rais Magufuli huyu huyu amefanikiwa kuvunja mfupa mgumu wa mtandao wa mafisadi nchini kwa kuwatumbua majipu vigogo na mafisadi wote waliokuwa huwezi kuwagusa awamu za nyuma na kuwapeleka mahakamani vigogo na mafisadi hao na wale wote waliokuwa na matumizi mabaya ya madaraka yao kupitia migongo ya ofisi na vyeo vyao.

Hali hiyo imepelekea heshima ya Serikali kurudi upya, imepelekea uimarikaji wa suala zima la uadilifu na uwajibikaji serikalini.

Huu ni utajiri mkubwa sana wa heshima aliyoileta Rais Magufuli ndani ya Serikali na kwa watumishi wote na hivyo kujenga imani ya kupungua kwa hati chafu nchini siku za usoni.

Rais Magufuli ameendelea kufanya maajabu kwa kuwafumbua macho Watanzania kuwa Taifa lilikuwa na watumishi hewa wengi tu na asilimia kubwa ya watumishi hewa hao walikuwa wakilipwa mishahara kila mwezi na wengine walifikia hatua kubwa ya kuweza hata kukopa mikopo ya fedha kwenye mabenki.

Rais Magufuli ameamuru watumishi wote hewa kubainishwa na kufutwa nchi nzima hali itakayopelekea kuokolewa kwa fedha nyingi ambazo zitaelekezwa kwenye matumizi ya kimaendeleo.

Katika kipindi cha miezi mitano tu tangu awe Rais, Magufuli amefanikiwa kuleta mabadiliko makubwa nchini ya uadilifu, uwajibikaji, ubanaji matumizi, uokozi na uimarishaji wa mapato ya makusanyo ya ndani.

Umefika wakati kwa watafiti kutokuishia kutoa tafiti za utajiri wa mali na fedha za watu (wakiwamo viongozi) bali waangalie hata na utafiti wa utajiri wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kupitia madaraka waliyowezeshwa na Wananchi kupewa Hakuna utajiri mkubwa kwa viongozi kama wao kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla wake, watafiti wamulike utajiri huu pia.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba +255 717 488 622

Ad