Kagame Ameahidi kuiga mfano wa Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli
Rais wa Rwanda Paul Kagame amelaumu Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutumia pesa ‘kiholela’ kutokana na mawaziri kufanya ziara za mara kwa mara kuhudhuria mikutano.
Amesema mawaziri wa nchi yake wanatumia chombo hicho kama njia ya kujinufaisha kwa kufanya ziara na kuhudhuria mikutano ya jumuiya hiyo isiyo muhimu.
Ameahidi kuiga mfano wa Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kutokomeza ufisadi huo wa kusitisha ziara za mawaziri alizotaja kuwa za kufuja mali ya taifa.
Akiongea katika mkutano wa faragha wa viongozi wa taasisi zote za serikali nchini Rwanda, Rais Kagame amesema suala la ufisadi nchini humo linachukua mwelekeo mpya na kasi ya ajabu na kwamba hawezi kuendelea kuvumilia.
Rais Kagame aidha amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imeanza kuwa ghali na mzigo kwa taifa lake akisema mawaziri katika mataifa wanachama wanatumia jumuiya hiyo kama chombo cha kuchota pesa kwa kubuni mikutano ya kila siku baadhi akiitaja kuwa haina umuhimu wowote.