Home » Afrika » Polisi mmoja nchini Zimbabwe kujibu mashtaka ya kumdhalilisha rais Mugabe

Polisi mmoja nchini Zimbabwe kujibu mashtaka ya kumdhalilisha rais Mugabe

09 March 2016 | Afrika

Polisi mmoja nchini Zimbabwe amefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumdhalilisha rais kwa kudai kuwa ni mzee sana kuongoza huku akimfananisha mke wake na wasichana wanaofanya biashara ya ngono.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Zimbabwe, vimeripoti kuwa, polisi huyo, Thompson Joseph Mloyi, amekana mashtaka dhidi yake, ambapo anadaiwa kuwa alitoa maneno ya kejeli dhidi ya rais Mugabe na mke wake, akiwa kwenye kambi moja ya jeshi na polisi.

Kwa mujibu wa maelezo ya mwendesha mashtaka wa Serikali, inadaiwa kuwa mtuhumiwa Mloyi bila ya kuwa amekerwa au kugombana na mtu, alitoa matamshi yaliyoashiria kumkejeli rais Mugabe na mke wake, akidai kuwa rais amemuoa mwanamke anayefanya biashara ya ngono.

Kesi za aina hii nchini Zimbabwe, ni kesi zilizozoeleka ambapo mara nyingi adhabu zake zimekuwa zikiishia kwa watuhumiwa kukaa jela kwa muda mfupi au kulipa faini kutokana na matamshi waliyoyatoa.

Polisi huyo ameachiliwa kwa dhamana ya dola za Marekani 100 na anatarajiwa kupandishwa tena kizimbani March 15 akikabiliwa na mashtaka ya kumtukana na kumdhalilisha mke wa rais Robert Mugabe.

Ad