Kwa Ujumla neno mtando lina maana ya mfumo au kikundi chochote kilichounganishwa. Hii ni njia mojawapo ya kubadilishana habari kati ya mifumo tofauti. TACAIDS inaratibu mitandao mbalimbali ya mapambano dhidi ya UKIMWI. Ifuatayo ni baadhi ya miandao hiyo:
- NETWO+: Ni Mtandao wa Taifa wa Wanawake wenye VVU/UKIMWI
- ICW: Ni Jumuiya ya Kimataifa ya Wanawake wanaoishi na VVU/UKIMWI
- MNEYOP+ : Ni Mtandao wa Taifa wa Vijana wenye VVU/UKIMWI
- TANGYWA+:Ni Mtandao wa Taifa wa Wasichana na Wanawake Vijana wanaoishi na VVU/UKIMWI Tanzania
- TANEPHA:Ni mtandao wa Asasi za Watu wanaoishi na VVU/UKIMWI Tanzania
- TANERELA :Mtandao wa Viongozi wa Dini wanaoishi au walioathiriwa na VVU/UKIMWI Tanzania
- NYP+ :Mtandao wa Vijana wanaoishi na VVU/UKIMWI
- NACONGO :Baraza la Taifa la Asasi zisizo za Serikali
- TAYOPA :Balozi wa Vijana wanaoishi na VVU/UKIMWI Tanzaniaa
- FONEPHAT :Mtandao wa Kitaifa wa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI
- NACOPHA:Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU/UKIMWI Tanzania
NACOPHA: Ni Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU/UKIMWI Tanzania ni asasi isiyo ya serikali iliyoanzishwa mwaka 2003 kwa madhumuni yaliyotajwa katika kifungu cha 2.4 cha katiba yao kama ifuatavyo: Kuwakutanisha watu wanaoishi na VVU/UKIMWI kwa madhumuni ya kuongeza ushiriki na kuongeza uwezo wao wa kushawishi katika majukumu yao katika kufanikisha mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI nchini Tanzania. NACOPHA ilianzishwa kama asasi mwavuli kwa mujibu wa dira na dhamira iliyotajwa katika katiba yao.
FONEPHAT: Ni Mtandao wa Kitaifa wa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI. Ni asasi mwavuli kwa ajili ya mitandao, vikundi na vyama vya watu wanaoishi na VVU/UKIMWI nchini. Ina jukumu la kuratibu mitandao ya WAVIU Tanzania. FONEPHAT ilianzishwa mwaka 20 Oktoba, 2007 mjini Dar es Salaam ambapo kwa sasa inaratibu mitandao 12 ya kitaifa ya WAVIU. FONEPHAT ina bodi na sekretariati.
TAYOPA: Ni Balozi wa Vijana wanaoishi na VVU/UKIMWI Tanzania. Ilianzishwa mwaka 1998 na kusajiliwa rasmi mwaka 2001. Inaongozwa na Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina. Vile vile ina kamati ya utendaji, maamuzi makuu hufanywa na mkutano mkuu ambao hukutana kila baada ya miaka mitano (5). TAYOPA ina matawi 4 katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Ruvuma na Rukwa. Jukumu kubwa la TAYOPA ni kuelimisha vijana walioko mashuleni na wasio kuwa mashuleni.
NACONGO: Ni chombo chenye jukumu la kuratibu na kujiratibu kwa asasi zisizo za serikali zinazofanya kazi Tanzania. NACONGO ilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 24 ya mwaka 2002, na kuzinduliwa rasmi mwaka 2003.
ICW: Ni Jumuiya ya Kimataifa ya Wanawake wanaoishi na VVU/UKIMWI. Ni mtandao wa kimataifa pekee unaoendeshwa kwa ajili ya na wanawake wenye VVU/UKIMWI. Ilianzishwa mwaka 1992 na wanawake 56 wenye VVU/UKIMWI duniani. Uanachama wa ICW ni huru na unawahusu wanawake wenye VVU/UKIMWI tu. ICU inahusu masuala na mahitaji yanayowakabili wanawake wanaoishi na VVU/UKIWM duniani kote na kuunda msingi wa philosophia ya asasi hiyo. Wanawake walikubaliana wasikate tama na ndio maana walianzisha jumuiya hiyo. ICW inajihusisha zaidi na uraghbishi kuhusu masuala ya wanawake.
NETWO+: Ni mtandao wa Taifa wa Wanawake wenye VVU/UKIMWI. Mtandao huu unafanya shughuli zake nchi nzima na unaendeshwa na wanawake wanaoishi na VVU/UKIMWI. Ulianzishwa mkoa wa Morogoro Decemba 28, 2002 na kusajiliwa rasmi Mei 30, 2003 kwa namba ya usajili SO11944. Ilianzishwa kwa madhumuni ya kuunganisha wanawake wanaoishi na VVU/UKIMWI na watu binafsi, vikundi na asasi zinazosaidia wanawake wenye mahitaji yanayohusiana na VVU/UKIMWI.
Lengo kuu la mtando huu ni kuongeza fursa ya wanawake wanaoishi na VVU/UKIMWI za kusikika na kushiriki katika shughuli za kidemokrasia zinazowezesha kusikika kwa haki zao na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadau na wahisani wengine.
TANERELA
TANERELA ni Mtandao wa Viongozi wa Dini Waishio na VVU au Walioathiriwa Binafsi na VVU/UKIMWI. Mtandao huu ulianzishwa kwa nia ya kuwawezesha viongozi wa Dini wanaoishi na VVU na wale walioathiriwa binafsi kufanya yafuatayo:
- Kuvunja ukimya na kuwa wazi kuhusu hali zao;
- kuondoa unyanyapaa binafsi – Kujinyanyapaa
- kuondoa mtazamo hasi wa kukana na kukataa ukweli wa hali halisi
- Kuondoa mawazo ya kudhani kwamba kuwa na VVU ni jambo la aibu
- kuwa chachu ya mabadiliko kiimani kwa wao wenyewe, kwa Jamii zinazowazunguka na kwa Taifa kwa jumla
- Makao Makuu ya TANERELA yako Dar es Salaam lakini pia ina matawi katika mikoa ya Dodoma, Kagera, Kigoma na Morogoro.
TANOPHA
TANOPHA ni mtandao wa Asasi za Watu Waishio na VVU/UKIMWI ambao ulianzishwa mwaka 2001 na kusajiliwa 2002. TANOPHA ilianza na asasi wanachama 22 na kwa sasa ina jumla ya wanachama 110 kwa nchi nzima.
TANOPHA Ilianzishwa kwa lengo la kuzipa nguvu na sauti na kuzisaidia asasi zinazoendeshwa na kungozwa na watu waishio na VVU katika Tanzania. Makao makuu ya TANOPHA yako Dar es Salaam
TANEPHA
TANEPHA ni mtandao wa watu waishio na VVU uliosajiliwa mwaka 2003 kwa lengo la kushirikiana na mitandao mingine ya ndani na nje ya nchi ili kuunganisha juhudi katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kuwa kituo cha Taarifa za kimataifa kwa WAVIU. Aidha TANEPHA inahusika pia na kufuatilia suala la upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU kwa walengwa.
TANGYWA+
TANGYWA+ ni mtandao wa wasichana na Wanawake vijana wanaoishi na VVU ulioanzishwa mwaka 2004 na kusajiliwa mwaka 2007. Mtandao huu unalenga kudhibiti maambukizo mapya ya VVU, kupigania haki za binadamu, afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake wa umri Mdogo.
Miongoni mwa shughuli za TANGYWA+ ni kuboresha hali za maisha ya wasichana kwa kutoa huduma zifuatazo:
- Misaada wa kimaadili, na kisaikolojia kwa wateja wake;
- Misaada ya lishe na vifaa vya shule kwa watoto yatima;
- kutoa maelekezo na ushauri kuhusu masuala ya tiba na matunzo kwa wagonjwa wa UKIMWI;
- Huduma za tiba, ushauri na matunzo nyumbani;
- mafunzo ya stadi za maisha kwa wasichana
- Hivi sasa mtandao huu unafanya kazi katika mikoa 8 ifuatayo katika Tanzania Bara: Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro,Morogoro, Mwanza, Singida na Pwani.
NNEYOP+
NNEYOP ni mtandao wa kitaifa wa Vijana Wanaoishi na VVU ulioanzishwa na kusajiliwa mwaka 2006 kwa ajili ya kuchangia juhudi za serikali za kudhibiti maambukizo ya VVU na UKIMWI nchini Tanzania.
Lengo la NNEYOP+ ni Kuunganisha vijana wanaoishi na VVU waweze kupigania haki zao na kutetea haki za vijana wanaoishi na VVU yakiwemo masuala ya unyanyapaa na ubaguzi. Aidha NNEYOP inatetea uimarishaji wa huduma za tiba, matunzo na misaada kwa vijana waishio na VVU na ushirikishwaji wao kwenye vyombo vya maamuzi.
|