Home » Biashara » Rais Dkt. Magufuli amezindua kiwanda cha kusindika matunda Bakhresa katika eneo la Mwandege,

Rais Dkt. Magufuli amezindua kiwanda cha kusindika matunda Bakhresa katika eneo la Mwandege,

10 October 2016 | Biashara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 06 Oktoba, 2016 amezindua kiwanda cha kusindika matunda kinachomilikiwa na kampuni za kitanzania za Bakhresa katika eneo la Mwandege, Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.

Kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda 13 vinavyomilikiwa na kampuni za Bakhresa vilivyopo Dar es Salaam na Pwani, kina uwezo wa kusindika tani 350 za matunda kwa siku, kimeajiri karibu wafanyakazi 1,000 na uwekezaji wake umegharimu takribani Shilingi Bilioni 261.

Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda hicho cha kwanza tangu aingie madarakani Rais Magufuli amempongeza Mwenyekiti wa kampuni za Bakhresa Bw. Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji huo na amesema Serikali yake itamuunga mkono yeye na wawekezaji wengine ambao wanazalisha ajira na kulipa kodi ipasavyo.

"Nawapenda wafanyabiashara wanaolipa kodi, nawachukia wafanyabiashara ambao hawalipi kodi, nawapenda wafanyabiashara wanaotengeneza ajira kwa watanzania, wewe umetengeneza ajira za watanzania, na umeendelea kutengeneza ajira kule mjini kwa wauza juisi na wengine, lakini pia unatengeneza ajira kwa wakulima.

Mtu akitengeneza nanasi zake anajua kuna soko la kupeleka, mtu akilima maembe yake anajua kuna soko la kupeleka" amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli ametoa miezi miwili kwa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme katika kiwanda hicho ili kupunguza gharama za uzalishaji zinazosababishwa na kutumia umeme unaozalishwa na majenereta.

Pia ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizotajwa na mmoja wa Wakurugenzi wa kampuni za Bakhresa Bw. Abubakar Said Salim Bakhresa zikiwemo kupatiwa gesi asilia kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kusindika matunda na urasimu unaosababishwa na wingi wa taasisi zinazodhibiti uzalishaji wa bidhaa.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa kampuni za Bakhresa kuwekeza katika uzalishaji wa sukari ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa bidhaa hiyo na amesema endapo kampuni hiyo ipo tayari Serikali itatoa eneo la kuzalisha miwa na kujenga kiwanda.

Mapema akitoa taarifa juu ya hali ya viwanda katika mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo amesema pamoja na viwanda viwili vya kampuni za Bakhresa vilivyopo Mkoani Pwani, Mkoa huo unavyo viwanda vingine 88 ambavyo vinazalisha bidhaa na vingine vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, vikiwemo viwanda viwili vikubwa Afrika Mashariki na Kati ambavyo ni kiwanda cha uzalishaji wa vigae (Tiles) na kiwanda cha kuzalisha nondo na vyuma vya madaraja vitakavyokamilika ifika Desemba mwaka huu.

Vingozi wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Mbunge wa Mkuranga Mhe. Abdallah Ulega na Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

06 Oktoba, 2016

Ad