Home » Afrika » Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa serikali ya DRC

Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa serikali ya DRC

24 May 2016 | Afrika

Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzisha upya haraka iwezekanvyo mchakato wa uchaguzi na kuelezea wasiwasi wake kuhusu kunyanyaswa na kutishiwa kwa wapinzani nchini humo.

Katika mkutano wa mawaziri 28 wa mambo ya nje, Umja huo unaitaka Serikali ya Congo kupiga hatua madhubuti kuelekea uchaguzi kutokana na mvutano wa kisiasa uliopo pamoja na kusisitizia haja na umuhimu wa mazungumzo ya kisiasa kati ya serikali na wadau wote kwa ajili ya makubaliano ya mpango wa wazi wa misingi ya kalenda inayoaminika na mahitaji ya kifedha.

Aidha, Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) kutangaza haraka iwezekanavyo kalenda ya uchaguzi itakayowaruhusu wadau mbalimbali wa kisiasa kutoa maoni juu ya hali ilivyo.

Sanjari na hayo, wanadiplomasia hao wameelezea wasiwasi wao kuhusu ongezeko ya visa vya kunyanyaswa na kutishiwa kwa viongozi wa upinzani kinyume na haki za binadamu ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, wanachama wa vyama vya kiraia, na wanaharakati wa haki za binadamu.

Umoja wa Ulaya unasisitizia jukumu la kila mmoja wa wadau wote, ikiwa ni pamoja na viongozi wa taasisi za haki na za kiusalama, kutenda katika heshima ya utawala wa sheria na haki za binadamu, vinginevyo watawajibika umeonya umoja huo.

Tayari, Uingereza imetoa tishio la "vikwazo" dhidi ya viongozi wa Congo watakaobanika kwa sera za "ukandamizaji" nchini humo, kama ilivyotangazwa juma lililopita na Mjumbe wake Maalum kwa ukanda wa Maziwa Makuu, Bi. Danae Dholakia.

Ad