Rais wa Tanzania amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kenya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, kando ya Mkutano Mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Mkoani Arusha, ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha mahusiano hususani katika masuala ya kiuchumi.
Baadhi ya maeneo waliyokubaliana kutilia mkazo katika mahusiano hayo, ni pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo inayounganisha nchi mbili ikiwemo ujenzi wa miundombinu, kukuza biashara na kuzalisha ajira kupitia viwanda.
Rais Uhuru Kenyatta amesema amefurahishwa sana kuona Rais Magufuli yupo tayari kuhakikisha nchi ya Kenya na Tanzania zinakuwa karibu, na miradi ya maendeleo inaharakishwa.
"Kwa sababu nia yetu sisi ni kuona maendeleo ambayo yatagusa mwananchi wa kawaida, tumalize umasikini, uchumi ukue, na hivyo hatuwezi kufanya tukiwa tumetengana" Amesisitiza Rais Kenyatta.
Kwa upande wake Rais John Pombe Magufuli, amesema Tanzania na Kenya zina kila sababu ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara hasa katika ujenzi wa viwanda utakaozalisha ajira kwa kuwa watu wake ni wamoja.
"Wazee wetu Mzee Kenyatta na Mzee Nyerere walijenga mazingira mazuri ya kuwa na nchi hizi mbili wakati wakipigania uhuru, sasa sisi vijana wao ni wakati wetu kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo" amebainisha Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amebainisha kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinajenga mahusiano na ushirikiano zinalenga kupata manufaa hayo ya kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake.
Ameutaja mradi mmojawapo kuwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda nchini Kenya kupitia Namanga, na akaongeza kuwa Tanzania itakapoongeza uzalishaji wa umeme na kuanza kuvuna gesi, itaiuzia pia Kenya, halikadhalika Kenya nayo itauza bidhaa zake Tanzania.
Kabla ya kukutana na Rais Kenyatta, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame, ambapo viongozi hao wamekubaliana kuzidisha mahusiano kati ya Tanzania na Rwanda ambapo Rais Magufuli amemhakikishia kuwa serikali yake itakamilisha ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge" ili kurahisha usafirishaji wa bidhaa na watu.
Rais Kagame amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake bora uliolenga kuimarisha uchumi, ikiwemo kuimarisha bandari ya Dar es salaam ambayo Rwanda inaitegemea na ujenzi wa Reli ya Kati ambayo pia ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa Rwanda.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiano, IKULU
Arusha
02 Machi, 2016