Home » Afrika » RAIS wa Gambia Yahya Jammeh amekataa kuondoka madarakani

RAIS wa Gambia Yahya Jammeh amekataa kuondoka madarakani

20 January 2017 | Afrika

RAIS wa Gambia Yahya Jammeh amekataa kuondoka madarakani kutoa nafasi ya kuapishwa kwa Adama Barrow hata baada ya makataa aliyopewa na Senegal kumalizika.

Barrow alipangiwa kuapishwa kuwa rais mpya Alhamisi, na wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi wako tayari kuingilia kati.

Rais huyo mteule sasa ametangaza kwamba ataapishwa katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal mwendo wa saa 16:00 GMT (saa moja Afrika Mashariki).

Ametangaza hayo kupitia mtandao wa Twitter na kuwaalika wananchi kuhudhuria.

Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz alikutana na Bw Jammeh kwa mazungumzo ya dakika za mwisho kabla ya kuondoka na kwenda Senegal kwa mazungumzo na rais Macky Sall.

Bw Barrow alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu mwezi uliopita na Bw Jammeh mwanzoni alikubali kushindwa lakini baadaye akapinga matokeo hayo.

Wanajeshi wa Senegal wamesalia kwenye mpaka wa nchi hiyo na Gambia, huku muda wa mwisho aliowekewa Bw Jammeh na Senegal kuondoka madarakani - saa sita usiku - ukipita.

Pendekezo la wanajeshi wa mataifa ya Afrika Magharibi kuingilia kati kumuondoa madarakani linaungwa mkono na Nigeria na nchi nyingine za kanda hiyo.

Mkuu wa majeshi ya Gambia Ousman Badjie amesema wanajeshi wake hawatapigana na wanajeshi wa Senegal iwapo wanajeshi hao wataingia nchini Gambia, shirika la habari la AFP limeripoti.

"Hatutahusika kijeshi, huu ni mzozo wa kisiasa," amesema.

"Sitashirikisha wanajeshi wangu katika mapigano ya kipuuzi. Nawapenda wanajeshi wangu."

Bw Jammeh ametawala Gambia tangu alipochukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1994.

Jumatano ilifaa kuwa siku yake ya mwisho madarakani lakini Bunge la nchi hiyo lilipitisha azimio la kumruhusu kuendelea kuongoza kwa miezi mingine mitatu.

Bw Barrow, ambaye anadaiwa kuwa katika harakati za kujiandaa kuapishwa kwenye "ardhi ya Gambia" siku ya Alhamisi, anasalia katika taifa jirani la Senegal.

Raia takriban 26,000 wa Gambia, ambao wanahofia kuzuka kwa mapigano, wamekimbia nchi hiyo na kutafuta hifadhi Senegal wiki hii.

Hayo yakijiri, maelfu ya watalii kutoka Uingereza na Uholanzi wanaendelea kuondolewa kutoka taifa hilo ndogo la Afrika Magharibi kwa ndege maalum za kukodishwa.

Gambia ni maarufu sana kwa watalii kutoka Ulaya kutokana na fukwe zake, hasa wakati wa majira ya baridi.

Mbona Jammeh hataki kuondoka madarakani?

Bw Jammeh awali alikubali kwamba Bw Barrow alishinda uchaguzi lakini baadaye akabadili msimamo wake na kusema hangeachia madaraka.

Alitangaza hali ya tahadhari ya siku 90 na kuhimiza "amani, utulivu na kufuatwa kwa sheria" baada ya kile alichosema ni udanganyifu uchaguzini.

Alisema tume ya uchaguzi ilifanya makosa mengi, na baadhi ya wafuasi wake walizuiwa kupiga kura vituoni.

Tume hiyo baadaye ilikubali kwamba baadhi ya matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na makosa, lakini ikasema makosa hayo hayangeathiri ushindi wa Bw Barrow.

Bw Jammeh amesema atasalia madarakani hadi uchaguzi mpya ufanyike.

Hatua yake ya kuendelea kung'ang'ania madaraka itahakikisha kwamba hashtakiwi kutokana na makosa aliyoyatenda wakati wa utawala wake.

Ecowas, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, iliipa Senegal jukumu hilo kwa sababu taifa hilo linaizunguka Gambia.

Kanali Abdou Ndiaye, msemaji wa jeshi la Senegal, amesema Ecowas iliamua kumuwekea Jammeh makataa ili kujaribu kupata suluhu ya kidiplomasia.

"Mambo yote yako tayari na wanajeshi wa Ecowas wako tayari kuingilia kati baada ya saa sita iwapo hatutapata suluhu ya kidiplomasia kwa mzozo huu wa Gambia," alisema.

Wanajeshi hao wa Ecowas wanasubiri Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe azimio la kutumiwa kwa "hatua zozote zile" kusaidia kuondolewa madarakani kwa Be Jammeh.

Wanajeshi wote wa Gambia ni takriban 2,500.

Hii inaifanya vigumu kufikiria ni vipi wanaweza kuwashinda wanajeshi wa kanda hiyo, anasema mwandishi wa BBC wa masuala ya usalama Afrika Tomi Oladipo.

Nigeria imesema imetuma ndege za kivita na ndege nyingine za kawaida, pamoja na wanajeshi 200 nchini Senegal. Wanajeshi hao walienda Senegal Jumatano asubuhi.

Meli za kivita za Nigeria pia zimewekwa tayari baharini.

Manowari moja iliondoka Lagos Jumanne na itakuwa na jukumu la kuwaokoa raia wa Nigeria walio nchini Gambia.

Ghana pia inachangia wanajeshi.

Source: BBC

Ad