'Niko tayari kumrithi mume wangu' Grace Mugabe.
Nchini Zimbabwe, suala la kumrithi rais Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka 93, linaendelea kuzua malumbani ndani ya chama tawala nchini humo. Mkewe, Grace Mugabe, alitangaza siku ya Jumapili, Novemba 5 kwamba yuko tayari kumrithi mumewe.
"Ninamwambia Mugabe: unapaswa kuniruhusu nichukua nafasi yako," mkewe, Grace Mugabe, alisema mbele ya maelfu ya watu katika uwanja wa mpira wa mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, tarehe 5 Novemba. "Usiogope. Ikiwa unataka kunipa nafasi yako, unipe kwa kwa nia njema. "
Rais Robert Mugabe alisikika siku moja kabla kuwa anaweza kumfukuza kazi Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa, ambaye anaonekana kama mmoja wa warithi wake na anaonekana kuwa mpinzani wa mke wa Rais Mugabe.
Emmerson Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 75, anayejulikana kwa jina maarufu la "mamba", tayari alipoteza nafasi yake ya Waziri wa Sheria mapema mwezi Oktoba. Grace Mugabe, mwenye umri wa miaka 52, alisema chama tawala hivi karibuni kitabadili sheria zake ili mwanamke awe makamu wa rais.
Uamuzi huo unaweza kumruhusu kuchukua nafasi ya Emmerson Mnangagwa na hivyo kufungua njia ya kumrithi rais wa zamani wa Afrika, ambaye anaongoza nchi yake kwa miaka 37.
Emmerson Mnangagwa aliteuliwa kuwa makamu wa rais mwaka 2014, akichukua nafasi ya Joice Mujuru, aliyepoteza nafasi yake baada ya kampeni ya Grace Mugabe ambaye alimshtumu kuwa anataka kumpindua rais Mugabe.
Siku ya Jumapili, Grace Mugabe pia alimshtumu Emmerson Mnangagwa kupanga njama, ikiwa ni pamoja na mapinduzi ya kijeshi wakati wa sherehe za uhuru. "Mwaka 1980, mtu huyu aitwaye Mnangagwa alitaka kufanya mapinduzi ya kijeshi. Alitaka kuchukua mamlaka ya rais. Alikuwa na uhusiano na wazungu", Grace Mugabe alisema.
Chama tawala, Zanu-PF, linakabiliwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu mrithi wa Robert Mugabe, ambaye alikataa kuteua mrithi. Rais Mugabe tayari ametangaza kwamba atawania muhula mwingine katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2018.
Na RFI