Home » Afrika » Ndege za kivita za jeshi la MONUSCO, DRC, zimefanya mashambulizi

Ndege za kivita za jeshi la MONUSCO, DRC, zimefanya mashambulizi

25 March 2016 | Afrika

Ndege za kivita za jeshi la MONUSCO nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, hii leo zimefanya mashambulizi kulenga ngome za waasi wa mashariki mwa nchi hiyo wa ADF, ambapo watu kadhaa wameripotiwa kufa na wengine kujeruhiwa.

Naibu kamanda wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa Mataifa nchini humo, MUNUSCO, Jean Baillaud amethibitisha kutekelezwa kwa operesheni hiyo ambayo amesema imetekelezwa kwa pamoja kwa kushirikiana na vikosi vya Serikali vya FARDC.

Jean, amesema kuwa kwenye opersheni waliyoitekeleza hii leo ndege zao zimefanikiwa kuteketeza makambi ya waasi wa ADF ambapo bado hawajapata idadi rasmi ya wapiganaji waliouawa na kwamba operesheni bado inaendelea.

Hii ni mara ya kwanza kwa tume ya umoja wa mataifa nchini DRC, MONUSCO, kushirikiana na vikosi vya Serikali, toka mwezi February tume hiyo ilipotangaza kusitisha ushirikiano wake, baada ya Serikali kuwataja majenerali wawili katika jeshi wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu wakati wakiwa kwenye operesheni za nje ya nchi.

Kundi la ADF lilianzisha uasi dhidi ya Serikali ya Rais Yower Museveni wa Uganda miaka 20 iliyopita lakini wakalizimika kukimbilia nchini DRC, ambapo toka mwaka 1995 kundi hilo linadaiwa kutekeleza makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Umoja wa mataifa ambao unakikosi cha wanajeshi elfu 20 nchini DRC, unalituhumu kundi la ADF kwa kutekeleza mauaji ya watu zaidi ya 500 wilayani Beni na Ituri toka mwaka 2014.

 

 

 

Ad