Home » Afrika » KESI YA MWANASIASA WA RWANDA INGABIRE YATUA MAHAKAMA YA AFRIKA

KESI YA MWANASIASA WA RWANDA INGABIRE YATUA MAHAKAMA YA AFRIKA

29 February 2016 | Afrika

Kesi ya mwanasiasa mfungwa raia wa Rwanda,Bibi  Victoire ingabire (42), itasikilizwa katika mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) yenye makao yake makuu jijini Arusha Ijumaa, Machi 4 2016.

Ingabire analalamika kuvunjiwa haki zake za msingi za binadamu na haki katika mchakato wa usikilizishwaji kesi yake nchini Rwanda kama ilivyoainishwa katika mkataba wa Afrika na haki za binadamu chini ya vifungu 1,3,5,7,10,11,28 and 19.

Anaiomba mahakama hiyo itoe amri ya kutupilia mbali maamuzi yote yaliyofikiwa na mahakama ya nchini kwake Rwanda ikiwemo kifungo chake.

Mwanamke huyo, aliyekuwa anawania uraisi na kiongozi wa sasa wa Rwanda Paul Kagame katika uchaguzi mkuu wa nchi  hiyo uliofanyika mwaka 2010, alishtakiwa na kisha mahakama kuu na mahakama ya juu ya Rwanda ilimhukumu kifungo cha miaka 8 hapo awali na baadaye miaka 15 jela ambapo miongoni mwa tuhuma zake zilikuwa ni pamoja kusambaza itikadi ya mauaji ya kimbari na kudharau usalama wa ndani ya nchi yake.

Ingabire aliondoka Rwanda kwenda Uholanzi muda mfupi kabla ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya  mwaka 1994  lakini alirejea nchini mwake mwaka 2010 kujishirikisha na siasa.

Katika usikilizwaji wa kesi hiyo mlalamikaji (bibi Ingabire) hatakuwepo mahakamani hapo bali atawakilishwa na mawakili wake.

Hata hivyo serikali ya Rwanda imesema kuwa haikubaliani na usikilizwaji wa kesi ya bibi Ingabire katika mahakama hiyo  ya Afrika kwa madai kuwa mashtaka ya mlalamikaji hayakidhi vigezo kupelekwa katika mahakama hiyo.

Kabla ya usikilizwaji wa kesi ya bibi Ingabire mahakama  pia Alhamisi inatarajiwa kusikiliza kesi nyingine ambapo shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na haki za binadamu la nchini Ivory Coast liitwalo APDH linaishtaki serikali ya IvoryCoast kuhusu ukiukwaji wa mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita wa nchi hiyo mwaka 2015.

Aidha mahakama hiyo pia itatazama maombi ya mwanamuziki maarufu raia wa Congo Nguza Viking, maarufu kama babu Seya, dhidi ya serikali ya Tanzania ambapo alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya udhalilishaji watoto kingono.

Majaji wa mahakama hiyo watapitia maombi ya mwanamziki huyo katika kikao cha faragha na kama yatafaa itapangwa tarehe ya kusikiliza shauri hilo.

Kikao cha kawaida cha 40 cha majaji wa mahakama hiyo ya Afrika ya haki za binadamu na watu pamoja na mambo mengine kinatarajiwa kuchunguza zaidi ya kesi 50 katika kikao chake kitakachoanza Jumatatu (Feb 29) hadi Machi 18  katika makao makuu ya mahakama hiyo jijini Arusha.

Mahakama hiyo ina majaji 11 walioteuliwa kutoka Nchi wanachama  wa umoja wa Afrika na hukutana mara 4 kwa mwaka katika vikao vyake vya kawaida.

Kwa mujibu wa Rais na mahakama hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani hadi hufikia tarehe 31 januari 2016 mahakama imepokea kesi 74 na kesi 25 kati ya hizo zimekwisha shughulikiwa huku kesi 4 zikipelekwa katika tume ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu Banjul, Gambia.

Mahakama ya Afrika  ilianzishwa mwaka 2006 na ilianza shughuli zake rasmi mwaka 2008.

KM/LC/MM/NI

Ad