Boutros Boutros-Ghali aliyefariki dunia hapo jana alikuwa nani?
Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, wa kwanza kutoka bara la Afrika, Boutros Boutros-Ghali aliyefariki dunia hapo jana alikuwa nani?
Alizaliwa Novemba 14 mwaka 1922 mjini Cairo Misri akitoka katika familia tajiri yenye ushawishi mkubwa na ya Wakristo wa dhehebu la Coptic.
Mwanafunzi mwenye kipaji, mwalimu, mwandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kisha katibu mkuu wa jumuiya ya nchi zinazozungumza Kifaransa (OIF), Mwenyekiti wa Baraza la Haki za Binadamu nchini Misri chini ya utawala wa Mubarak, Boutros Boutros-Ghali, hajaisahau nchi yake na bara la Afrika.
Uongozi ulikuwa damuni kwa Bwana Ghali, kwani Baba yake Yusuf Ghali aliwahi kuwa waziri wa fedha wa Misri na ingali babu yake alikuwa waziri mkuu wa taifa hilo kuanzia mwaka 1908 hadi alipouawa mwaka 1910.
Boutrous-Ghali aliyekuwa mtanashati na mzungumzaji wa lugha mbalimbali ikiwemo Kiingereza, kifaransa na Kiarabu alisomea sheria kwenye chuo kikuu cha Cairo na baada ya kuhitimu mwaka 1946 akahamia Ufaransa kwa miaka minne akijikita katika kusoma masuala ya kidiplomasia na uchumi na hatimaye kupata shahada ya uzamivu au Phd ya sheria za kimataifa kwenye chuo kikuu cha Paris mwaka 1949.
Alikuwa miongoni mwa wajumbe wa tume ya Umoja wa mataifa ya sheria za kimataifa kuanzia mwaka 1979-1992, na ndipo alipopata fursa ya kuyafahamu vizuri masuala ya Umoja wa Mataifa ambayo baadaye yalimpa fursa ya kutumikia Umoja huo hapo baadaye.
Lakini kwanza alitumikia taifa lake kama waziri wa mambo ya nje enzi za utawala wa Rais Anwar Sadat. Na alipoingia madarakani Rais Hosni Mubarak alimpandisha cheo na kumfanya kuwa naibu waziri mkuu wa masuala ya kimataifa hadi pale alipopata mwaliko rasmi wa kuungoza Umoja wa Mataifa mwinshoni mwa mwaka 1991.
Bwana Boutros-Ghali aliitikia wito na tarehe 3 Disemba mwaka 1991 aliapishwa Rasmi na Rais wa baraza kuu wakati huo Samir S. Shihabi wa Saudi Arabia ili kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Boutros Boutros-Ghali alichangia kukomesha migogoro mmbalimbali barani Afrika na katika mataifa mengine kama vile, Yougoslavia ya zamani na kutafutia suluhu mgogoro kati ya Israel na Palestina.
Boutros Boutros-Ghali amefariki akiwa na umri wa miaka 93. Afrika itamkumbuka zaidi kwa mchango wake wa kutafutia ufumbuzi migogoro mbalimbali barani humo.