Home » Afrika » Adhabu kali ya kifungo gerezani kwa mtu yeyote atakaye oa mtoto

Adhabu kali ya kifungo gerezani kwa mtu yeyote atakaye oa mtoto

22 July 2016 | Afrika

Nchi ya Gambia juma hili, imepitisha sheria inayokataza ndoa za utotoni na kutangaza adhabu kali ya kifungo gerezani kwa mtu yeyote atakaye kiuka sheria hii.

Chini ya sheria hii mpya, mwanaume atakae oa msichana wa chini ya umri wa miaka 18, atakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela, ambapo wazazi wake watahukumiwa kifungo cha miaka 21 jela, huku imam atakayebainika kufungisha ndoa hiyo atahukumiwa kifungo kama hicho.

Sheria hii pia, inasema mtu yeyote atakayebainika, kuwa alikuwa anafahamu kuna mtu amemuoa msichana wa chini ya umri wa miaka 18 na kuacha kuripoti tukio hilo kwa mamlaka husika, atakabiliwa na kifungo cha miaka 10 jela.

Sheria hii imepitishwa ikiwa ni majuma machache yamepita, toka rais Yahya Jammeh, atangaze nia yake ya kuidhinisha sheria hiyo, ambayo wakati fulani alisema haiendani na sheria za kiislamu kwenye taifa lake ambalo asilimi 95 ni waislamu ambayo ni sawa na watu milioni 1 na laki 8.

Mwezi December mwaka 2015, wabunge walipitisha pia, muswada wa sheria inayokataza ukeketaji wa wanawake, na kutoa adhabu ya hadi miaka mitatu kwa mtu atakayekiuka sheria hiyo.

Hivi karibuni, mahakama kuu ya Tanzania, ilitoa hukumu katika kesi ya kihistoria, ambapo ilidai ndoa yoyote ya chini ya umri wa miaka 18 ni batili na ni kunyume na katiba ya nchi, hukumu ambayo ilipongezwa na wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika yanayotetea wasichana.

Ad