Home » Uchaguzi » Elimu ya Mpiga Kura

Elimu ya Mpiga Kura

19 October 2016 | Uchaguzi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa fursa kwa vyombo vya habari kuialika kutoa Elimu ya Mpiga Kura kwa Wamiliki,Wahariri na wafanyakazi wa vyombo hivyo ili kukuza uelewa juu ya sheria, kanuni, na taratibu zinazoongoza na kusimamia uendeshaji wa uchaguzi na kufahamu majukumu ya Tume hapa nchini.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani ofisini kwake wakati akitoa tathmini juu ya Elimu ya Mpiga Kura inayotolewa na Tume hivi sasa hapa nchini.

Alisema NEC imejipanga kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima na iko tayari kupokea maombi ya kwenda kutoa elimu hiyo kwa Wamiliki,Wahariri na wafanyakazi wote wa vyombo vya habari ili kukuza uelewa katika tasnia hiyo.

Niwaombe Wakuu na wamiliki wa vyombo vya habari, wafahamu kuwa Tumeanzisha programu ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura,mtualike tuje tuzungumze na ninyi vyombo vya habari kimoja baada ya kingine” alisema Bw. Kailima na kufafanua kuwa:

“Sisi tunataka kuzungumza na wewe mmiliki wa chombo na watumishi wako na viongozi wenzako wote ili tukueleweshe kuhusu Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, utaratibu mzima wa uchaguzi na uijue Tume ili unapoandika ujue ninachoandika si cha kubahatisha”

Bw. Kailima alisema elimu kwa vyombo vya habari pia itaviwezesha kuwa na uelewa mpana juu ya masuala mbalimbali ya uchaguzi na kutoa changamoto kwa mtendaji huyo wa NEC pindi anapopata nafasi ya kuzungumza nao.

Katika kutekeleza mkakati endelevu wa kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, Bw. Kailima ameanza kutoa elimu hiyo kupitia televisheni mbalimbali nchini na kwamba yuko tayari kuzungumza na vyombo mbalimbali kutekeleza mkakati huo.

Kwa upande mwingine, Bw. Kailima amewataka Watanzania wakisikia kuna maonesho au mkutano wowote rasmi ambapo Tume inashiriki wafike banda la NEC waulize maswali wapate ufahamu na watapata uelewa mkubwa juu ya mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza kwa nyakati tofauti, Bw. Kailima alisema NEC itahakikisha inatumia maonesho, mikutano na mikusanyiko mbalimbali ikiwemo mikutano ya kidini ili kutoa Elimu ya Mpiga Kura ikiwemo shule za sekondari nchini.

Alisema lengo kuu la kutekeleza hayo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 wananchi wawe wamepata uelewa wa kutosha kuhusu taratibu za uchaguzi na kufahamu majukumu ya Tume ili kupunguza malalamiko na upotoshaji unaofanywa katika kipindi cha uchaguzi.

Tayari Bw. Kailima ameshatoa Elimu ya Mpiga Kura kupitia televisheni za Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na Televisheni ya Afrika Mashariki (EATV) na amesema NEC anajipanga kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Aidha,alisema NEC itatoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuziomba Asasi za Kiraia zinazoweza kutoa Elimu ya Mpiga Kura kutuma maombi ili kupatiwa vibali vya kutoa elimu hiyo kwa umma.

Ad