RAIS DKT. MAGUFULI AWAAPISHA BALOZI WA TANZANIA NCHINI CANADA NA KATIBU TAWALA WA MKOA WA TABORA LEO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Mei, 2018 amemuapisha Mhe. Alphayo Japani Kidata kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na Bw. Msalika Robert Makungu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora.
Mhe. Balozi Kidata ambaye pia ataiwakilisha Tanzania nchini Cuba anachukua nafasi iliyoachwa na Mhe. Balozi Jack Mugendi Zoka ambaye amemaliza muda wake, wakati Bw. Makungu anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Thea Ntara ambaye amestaafu.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa uteuzi huo na kuwataka kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kwa manufaa ya Taifa.
Mhe. Rais ameelezea kusikitishwa kwake na kutotekelezwa kwa maagizo aliyoyatoa kwa Mabalozi wote kumpa taarifa juu ya utendaji wao wa kazi na manufaa ambayo Tanzania imeyapata kwa uwepo wa kila Balozi katika nchi aliyopangiwa kila robo mwaka.
“Nataka nijue katika kipindi ambacho Mhe. Balozi ameteuliwa kuiwakilishi Tanzania katika nchi fulani, nchi imenufaikaje na uwepo wake kwenye nchi ile? Kuteuliwa sawa lakini sio lazima ukae katika ubalozi huo kwa kipindi chote ulichopangiwa, ukishindwa kuleta manufaa unarudishwa na huko anapangiwa mtu mwingine atayeleta manufaa kwa nchi” amesema Mhe. Rais Magufulli.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kufanya kazi nzuri katika sekta ya elimu na afya lakini ameelezea kutoridhishwa na utendaji katika sekta maji na ardhi kutokana na usimamizi mbaya wa miradi mingi ya maji na usimamizi mbaya wa masuala ya ardhi na mipango miji.
Mhe. Rais Magufuli amesema tangu mwaka 2010 Serikali imetoa Shilingi Bilioni 109 kwa ajili ya miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, lakini uchunguzi umeonesha miradi iliyotekelezwa ipasavyo na kuonesha thamani halisi ya fedha zilizotumika, ni ya Shilingi Bilioni 17 tu.
Kufuatia hali hiyo Mhe. Rais Magufuli ameagiza wataalamu wote wa idara za maji katika halmashauri zote nchini wasimamiwe moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na wataalamu wa ardhi na mipango miji katika halmashauri zote nchini wasimamiwe na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa na idara hizo na kuwawajibisha wahusika pale mradi unapotekelezwa visivyo.
“Sasa hivi kila mahali watu wanalalamikia maji, wabunge wanalalamika, wananchi wanalalamika, Serikali imetoa fedha lakini miradi haitoi maji, ukichunguza miradi hii inasimamiwa na wahandisi wa maji wa halmashauri ambao Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambaye ana wataalamu wa maji hana uwezo wa kuwawajibisha, wahandisi wanawajibika kwa madiwani, sasa hatuwezi kwenda kwa mtindo huo.
“Vivyo hivyo kwenye ardhi kuna matatizo mengi ya ardhi na mipango miji, watu wanadhulumiwa ardhi, ugawaji wa viwanja ni matatizo, maafisa ardhi na mipango miji wanachelewesha vibali vya ujenzi, huku nako Katibu Mkuu wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi hana mamlaka ya kuwachukulia hatua, hili nalo tatizo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kukutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwele na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi kutengeneza muundo utakaozingatia maelekezo hayo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Mei, 2018