Rais Magufuli amewashukuru Madaktari na Wauguzi wanaomhudumia Mama yake na wagonjwa wengine nchini na amewaombea
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 30 Desemba, 2018 ameungana na Waumini wa Kanisa la Mtakatifu Petro, Parokia ya Oysterbay Jijini Dar es Salaam kuadhimisha sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Joseph.
Misa Takatifu ya kuadhimisha sherehe hiyo imeongozwa na Paroko Msaidizi, Padre Bathlomeo Bachoo ambaye amesisitiza umuhimu wa jamii kujenga familia bora, inayochapa kazi na inayomcha Mwenyezi Mungu.
Padre Bachoo pia amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kutanzua sintofahamu kuhusu mafao ya wastaafu na ametoa wito kwa familia zitakazonufaika na uamuzi huo kutumia mafao hayo kujenga umoja na kuimarisha familia zao.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemjulia hali Mama yake mzazi Bibi. Suzana Magufuli ambaye anapatiwa matibabu Jijini Dar es Salaam tangu miezi mitatu iliyopita baada ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi (Heart Stroke).
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameongoza maombi ya kumuombea Mama yake pamoja na watu wote wanaokabiliwa na maradhi na kuwatakia heri ya mwaka mpya wa 2019.
Vilevile amewashukuru Madaktari na Wauguzi wanaomhudumia Mama yake na wagonjwa wengine nchini na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu heri na fanaka katika majukumu yao ya kunusuru maisha ya watu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
30 Desemba, 2018