Home » Tanzania » Watanzania wahamasishwa kujitokea kupata chanjo ya Homa ya Ini

Watanzania wahamasishwa kujitokea kupata chanjo ya Homa ya Ini

21 December 2018 | Tanzania

Wananchi watakiwa kupima afya zao mara kwa mara kubaini magonjwa mbali mbali nyemelezi ikiwemo ungojwa wa homa ya ini ambao watu wengi bado hawana uelewa nao.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Chanjo ya Homa ya Ini kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt Kandali Samuel alipokuwa katika Chuo cha Sayansi ya Afya Cha Mtakatifu Jospeh Jijini Dar Es Salaam wakati wa uchunguzi na utoaji wa chanjo ya homa ya ini kwa wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho.

Akizungumza na wanahabari, Dkt. Kandali Samuel amesema kuwa wamefika katika Chuo hicho kutoa huduma ya uchunguzi wa virusi aina ya Hepatitis B vinavyosababisha ugonjwa wa Homa ya Ini.

 “Kirusi cha Hepatitis B ni miongoni mwa virusi vinavyoshambulia ini na kusababisha homa ya ini, kirusi hiki ni hatarai na kinaweza kupelekea magonjwa mbalimbali ya ini ambayo hudhoofisha ini na kusababisha magonjwa ya ziada na kushusha utendaji kazi wa ini” amesema Dkt. Kandali.

Hata hivyo Dkt. Kandali amesema kuwa mtu anaweza kuishi muda mrefu bila kugundua kuwa ana ugonjwa huo ambao dalili zake huwa hazijionyeshi kwa kipindi cha muda mfupi kulingana na kinga ya mtu. “Virusi hivyo huweza kusabababisha athari kubwa kwenye mwii wa binadamu na hadi kusababisha saratani ya ini” alisema Dkt. Kandali.

Dkt Kandali amesema kuwa takwimu za ugonjwa huo nchini zinaonyesha kuwa asilimia 4.4 ya watanzania wanaishi na maambukizi ya virusi vya Hepatitis B ambapo kati ya watu 20 mmoja ana virusi hivyo.

Akifafanua namna maambukizi ya ugonjwa huo hutokea, Dkt Kandali amesema kuwa ugonjwa wa homa ya ini huambukizwa kupitia maji maji na damu kutoka kwa mtu mwenye virusi vya Hepatitis B kwenda kwa mtu mwingine kwa njia ya kujamiina, kutumia vitu vyenye ncha kali kwa zaidi ya mtu mmoja au kutoka kwa mama mzamzito kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.

Aidha Dkt. Kendali amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaandaa mwongozo ambao utawezesha uchunguzi wa mgonjwa toka amepata maambukizi ili kuwezesha tafiti kubaini athari nyinginezo zinazoweza kuambatana na ugonjwa huo huku taasisi ya Saratani Ocean Road kwa sasa ikijikita katika utoaji wa kinga dhidi ya ugonwja huo.

“Watu wengi wanajua kazi ya ini ni kuchuja sumu, endapo ini likifeli hata ufanyaji kazi ya kuchuja sumu na madawa mwilini pia huathirika. Ini pia linachangia katika kutengeneza chembe nyekundu za damu kwa kutengeneza protini” Alisema Dkt. Kendali na kuwataka wananchi kuchunguza afya zao mara kwa mara.

Naye Mhadhiri kutoka Idara ya Mikrobailojia na Kinga chuoni hapo Profesa Fred Mhalu amesema kuwa kinga ni bora zaidi kuliko tiba kwani hutusaidia kwa kutukinga na maradhi yanayoletwa na vimelea au virusi nyemelezi.  “Ugonjwa wa ndui umekwisha na polio karibia inakwisha ni kutokana na utaratibu mzuri wa kingatiba uliowekwa wa kujikinga na magonjwa hayo kupitia chanjo” alifafanua Profesa Mhalu.

Kwa upande wake Bw. Bonaventure Mattogo, Rais Serikali ya wanafunzi chuoni hapo amesema kuwa zoezi hilo limepokelewa kwa furaha na wanafunzi wote na kuishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kuja na mpango huo.

“Magonjwa yanayosababishwa na virusi yapo mengi lakini ugonjwa huu wa homa ya ini chanjo  yake inapatikana, ni vyema watu wakajitokeza katika hospitali zetu kupata chanjo hii ambayo hutolewa mara moja ambayo hukupa ulinzi dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini kwa kipindi cha maisha yako yote” alisema Bw. Mattogo

Mwisho

Ad