Jeshi la Afrika Kusini limekashifu shambulio wanajeshi wa kulinda amani Darfur
Jeshi la Afrika Kusini limekashifu vikali shambulio la kushtukiza lililotekelezwa kuwalenga wanajeshi wake wa kulinda amani kaskazini mwa jimbo la Darfur nchini Sudan, na kuongeza kuwa kitendo hicho hakikubaliki.
Jeshi la Afrika Kusini limetoa kauli hii wakati huu likithibitisha kuwa wanajeshi wake wawili waliuawa juma lililopita kwenye shambulio la kushtukiza na kuwataja waliouawa kwenye shambulio hilo kuwa na Koplo Msolisi Edward na Brigedia Jenerali Solani Mabanga.
Msafara wa wanajeshi wa Afrika Kusini uliokuwa ukitoa ulinzi kwa magari ya kutoa misaada, ulishambuliwa jimboni Darfur wakati ulipokuwa ukirejea kwaajili ya kubadilishana doria kati yake na wanajeshi wa Rwanda.
Shambulio hili linajiri ikiwa ni siku chache tu, toka wizara ya ulinzi nchini humo itangaze kuwa itawaondoa wanajeshi wake ifikapo mwezi April mwaka huu.