Msanii nyota wa Tanzania Diamond Platnumz afikisha mashabiki milioni 5 youtube
Mwanamuziki mashuhuri nchini Tanzania, Diamond Platnumz amepiga hatua nyingine kubwa katika kazi yake ya muziki.
Diamond kwa jina halisi Naseeb Abdul amekuwa mwanamuziki wa kwanza kusini mwa jangwa la sahara kupata watazamaji milioni tano katika mtandao wa Youtube, kupitia chaneli yake ya youtube.
Kwa karibu anafuatwa na Davido akiwa na watazamaji milioni 2.38, Burna Boy milioni 1.82 na Wizkid milioni 1.68.
Mafanikio haya ya sasa ya Diamond yanakuja yakifuata rekodi aliyoiweka mwaka jana (2020) baada ya wimbo wake maarufu 'Waah' aliomshirikisha mwanamuziki wa Koffi Olomide wa DRC kutazamwa na watu milioni 8 ndani ya saa chache baada ya kibao hicho kutoka, na kuvunja rekodi iliyowekwa na mwanamuziki wa Nigeria Davido baada ya kibao chake 'Fem' kuwavuta watazamaji milioni moja ndani ya saa 9 tangu kibao hicho kilipoachiwa.
Rekodi nyingine iliyowekwa na mwimbaji huyo ni kuwa msanii wa kwanza kusini mwa jangwa la Sahara kuwa na watazamaji bilioni moja youtube.
Kwanini Diamond Platinumz anawafuatilia sana watazamaji wake Youtube?
Katika kipindi cha miaka 10 iliopita, mwanamuziki huyo alieshinda mataji kadhaa amekuza muziki wa bongo fleva kuwa maarufu - muziki wa kipekee wa Tanzania unaotoa nyimbo za kimapenzi zilizochanganywa na midundo ya kisasa inayotokana na muziki wa jadi wa taarab kutoka pwani ya Afrika.
Diamond Platinumz ni mwanamuziki alie na bidii na maonyesho yake huvutia mashabiki wengi, kulingana na DJ Edu, ambaye amekuwa mtangazaji wa kipindi cha runinga cha kila wiki cha muziki wa Afrika cha BBC.
- Huku akiwa na asilimia 43 ya mashabiki miongoni mwa raia milioni 55 nchini Tanzania wanaoweza kuingia katika mtandao, kupitia simu aina ya smartphones, kuna mashabiki wengi wanaopenda muziki wa bongo fleva walio tayari kusikiliza muziki wake wa mapenzi.
Wanamuziki wengine kama Harmonize pia nao wamebobea katika YouTube.
Je Views bilioni moja ni nyingi kiasi gani katika YouTube?
Ni vigumu kubaini umuhimu hasa wa nambari bilioni moja, ikizingatiwa kwamba Diamond Platinumz ana wafuasi wengi katika mtandao wa Instagram ikilinganishwa na wafuasi wake katika YouTube ambao ni milioni 9.7 ikilinganishwa na milioni 3.7.
DJ Edu anasema kwamba Instagram ni mtandao wenye ushawishi mkubwa kuhusu mtindo wa maisha na majukwaa mengine kama vile TikTok , ambayo inaruhusu sekunde 30 za hakimiliki ya utumizi wa bure wa nyimbo - ni njia nzuri ya kuwanasa wafuasi vijana.
''Nyimbo nyengine zinasambaa sana kupitia TikTok , kama wimbo mpya wa Diamond Platinumz kwa jina Quarantine'', anasema.
/bbc