Home » Makala » WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada ya wakazi wa vijiji vya Mtondo na Nanjaru

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada ya wakazi wa vijiji vya Mtondo na Nanjaru

29 February 2016 | Makala

WAZIRI APOKEA MISAADA KWA WALIOPATWA NA MAAFA RUANGWA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali kwa ajili ya wakazi wa vijiji vya Mtondo na Nanjaru wilayani Ruangwa mkoani Lindi ambao nyumba zao ziliezuliwa na upepo Januari mwaka huu.

Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo  (Jumapili, Februari 28, 2016), Waziri Mkuu alisema maafa huwa yanakuja bila kutarajiwa na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wadau waliotoa misaada ya chakula, magodoro, mashuka, vitenge, mabati na mbegu za mazao.

Aliwataja wadau hao kuwa ni benki ya NMB, NSSF, wakazi wa Ruangwa na marafiki wa Ruangwa waishio Dar es Salaam ambao walifika kukabidhi misaada hiyo.

 
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili katika mikoa ya Mtwara na Lindi  kukagua athari za mafuriko, hatua zinzochukuliwa za utoaji misaada kwa waathirika na kuwapa pole wananchi walioathirika na mafuriko hayo, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio mabondeni wahame kwa sababu mvua kubwa bado zinakuja.

 

"Jambo hili si mipango ya mtu binafsi na sote tunajua kwamba tunahitaji mvua kwa ajili ya mazao lakini safari hii zimekuja zaidi ya kiwango cha kawaida. Mamlaka ya hali ya hewa imeshasema kuwa mvua kubwa zaidi zinakuja ifikapo Machi mwaka huu", alisema.

 

Ili kuepusha maafa zaidi, kuanzia sasa, wale waliojenga mabondeni wanapaswa wahame. Pia nawasihi wananchi wachukue tahadhari wakiona mvua inakuja na upepo mkali wasikae ndani ya nyumba sababu hapa kijijini tumempoteza mzee wetu mmoja ambaye aliangukiwa na nyumba baada ya nyumba yake kuangukiwa na mti kutokana na mvua hizo," aliongeza.

 

Kwa mujibu taarifa ya maafa iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Bi. Mariam Mtima, mvua zilizonyesha kati ya Januari na Februari mwaka huu zilisababisha nyumba 393 kuezuliwa na nyingine kubomoka na kuacha wakazi wa vijiji hivyo bila makazi.

 

"Zahanati ya kijiji cha Mtondo iliezuliwa paa, daraja la mto Muhuru limebomoka na halipitiki kabisa na ekari 1,186 za mashamba ya wananchi zimesombwa na maji. Mazao yaliyoathirika ni mahindi, muhogo, mikorosho, mtama, ufuta, kunde, mpunga na mbaazi," alisema Mkuu huyo wa wilaya katika taarifa yake.

Alivitaja vijiji vingine ambavyo mafuriko hayo yaliharibu mashamba ya wananchi kuwa ni Nambilanje, Mkaranga, Namkatila, Chinongwe A, Likwachu, Nauname na Mbekenyera.

 

Alisema hali hiyo imesababisha upungufu mkubwa wa chakula wilayani humo na sasa hivi wanahitaji tani 1,133 za chakula aina wanga ambazo anataraji zitatosheleza mahitaji kwa mwezi Machi 2016.

 

 (mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, FEBRUARI 28, 2016.

 
Ad