Home » Washirika » Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango afanya ziara ya kushitukiza Ofisi za TRA Kigamboni

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango afanya ziara ya kushitukiza Ofisi za TRA Kigamboni

11 July 2017 | Washirika

Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam

Wakazi wa Kigamboni mkoani Dar es Salaam, wameiopongeza Serikali kwa kusimamia vizuri masuala ya kodi na kwamba wako tayari kuiunga mkono Serikali kwa kulipa kodi kwa hiari ili iweze kutimiza malengo yake ya kuwahudmia wananchi kimaendeleo.
 
Wametoa kauli hiyo wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipofanya ziara ya kushitukiza kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Kigamboni, ili kujionea zoezi la wakazi wa Mji huo wanavyolipa kodi ya majengo na kutembelea baadhi ya vituo vya mafuta ili kuona kama wamiliki wanatoa risiti ipasavyo kwa wateja wao.
 
Wakitoa maoni yao kuhusu zoezi hilo la kulipa kodi ya majengo, wakazi hao wameelezea kuridhishwa na huduma wanayopata kutoka kwa wafanyakazi wa TRA na kuiomba Serikali iangalie namna ya kuongeza muda wa kulipa kodi hiyo kutokana na mwamko mkubwa uliopo hali inayoonesha kuwa huenda baadhi yao wasikamilishe zoezi hilo ifikapo Julai 15 Mwaka huu.
 
“Ninampongeza sana Mhe. Rais kwa kutupatia Waziri huyu (Dkt. Mpango), anajibu vizuri na kwa kuamua kututembelea, pia wafanyanyakazi wa TRA wanatuhudumia vizuri sana, tunakushukuru Mhe. Waziri” alisema kwa furaha
Bi. Mary Laizer, Mkazi wa Kigamboni.
 
Akizungumza na wakazi hao, Dkt. Philip Mpango amewafikishia watanzania salaam na pongezi za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna walivyoitikia wito wa kulipa kodi na kwamba hatua hiyo itaiwezesha Serikali kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu, maji na miundombinu mbalimbali kutokana na mapato ya kodi hizo
“Mkiona barabara zinajengwa, tunafanya jitihada kuongeza dawa hospitalini, kulipa wanajeshi wetu ili watulinde usiku wakati sisi tumelala, inatokana na nguvu tunayoipta kutoka kwenu kupitia kodi” alisisitiza Dkt. Mpango.
 
Alisema kuwa amekwenda Kigamboni kuwashukuru wakazi wa Mji huo kwa mwitikio wao mkubwa wa kulipa kodi hususan ya majengo kwa hiari na kuangalia changamoto zinazokabili zoezi la ukusanyaji kodi ikiwemo msongamano mkubwa wa watu na kugundua uhaba wa baadhi ya vitendeakazi kama vile kompyuta na watumishi
Kwa upande wake Meneja Ukaguzi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Beatus Nchota, alitoa wito kwa Watanzania kuendeleza moyo huo wa kulipa kodi kwa hiari hata kwenye kodi nyingine za biashara ili Serikali iweze kupata mapato ya kutosha ya kuwahudumia wananchi wake.
 
Wakati huo huo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameamuru kufungwa kwa kituo cha Mafuta cha Mawenzi kilichoko Kigamboni hadi mmiliki wake atakaporekebisha kasoro baada ya kubaini kuwa mashine maalumu za Kieletroniki zilizofungwa kwenye pampu za mafuta kwa ajili ya kutolea risiti hazitumiki, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
 
Akiwa katika kituo hicho cha mafuta, Dkt. Mpango alishuhudia mashine mbili za kielekroniki zikiwa hazifanyikazi badala yake wahudumu wanatumia mashine za kieletroniki za kawaida ambazo haziwezi kupima kiwango cha mafuta kinachotoka kwenye pampu za mafuta hatua mabayo inaikosesha serikali mapato yake halisi.
 
Msimamizi wa Kituo hicho Bw. Yusuph Abbass alisema kuwa mashine hizo zote mbili zilipata hitilafu juma moja lililopita na kulazimika kutumia mashine za EFD za kawaida jambo ambalo lilipingwa na Waziri Dkt. Mpango kwa kuwa ni kinyume cha taratibu na sheria na maelekezo ya Serikali.
 
Kufuatia hatua hiyo Dkt. Mpango ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvikagua na kuvifunga vituo vyote vya mafuta nchini ambavyo havijafunga machine hizo za kutolea risiti kama wamiliki wake walivyoagizwa na Serikali tangu mwaka jana hatua ambayo inaikosesha Serikali mapato yake.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Philip Isdor  Mpango  (Mb)  akiongea na mmoja wa wananchi (anayemuonesha karatasi ) waliofika kulipa kodi ya majengo katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) – Kigamboni, ambapo alieleza kuridhishwa na utendaji wa watumishi katika mamlaka hiyo.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), aliyevaa miwani na kukunja mikono, akiwa amejichanganya katika kundi la wakazi wa mji wa Kigamboni waliojitokeza kulipa kodi ya majengo katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania-Kigamboni, akiwa na lengo la kuchunguza namna wananchi wanavyopata huduma. 
 
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango  (Mb) (kulia) akisalimiana na mmoja wa wakazi wa Mji wa Kigamboni waliojitokeza kulipa kodi katika Ofisi za mamlaka ya mapato Tanzania TRA-Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Msaidizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Hussein Shah alipotembelea ofisi za Mamlaka hayo, Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango  (Mb) (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Ukaguzi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA-Bw. Beatus Nchota (kulia) wakati Dkt. Mpango alipotefanya ziara ya kushitukiza katika Ofisi za TRA-Kigamboni, Jijini Dar es Salaam kujionea utendaji kazi wa Mamlaka hayo wakati wananchi wakijitokeza kwa wingi kulipa kodi ya majengo. Katikati ni Afisa wa (TRA) Bw. Theraphin Mbwambo.
 
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Philip Isdor  Mpango  (Mb), akiwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Kigamboni waliojitokeza kulipa kodi ya majengo na kutoa rai kwa wananchi kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari ili kufikia uchumi wa viwanda na kuendesha huduma za jamii.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb), akimsikiliza Msimamizi wa Kituo cha Mafuta cha Mjimwema, Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Bw. Yusuph Abbass baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika kituo hicho na kubaini kuwa mashine za kielektroniki za kutolea risiti hazitumiki.
 Moja kati ya  Mashine mbili za Kielektroniki zilizofungwa katika Kituo cha Mafuta cha Mjimwema Kigamboni, Jijini Dar es Salaam lakini hakitumiki baada ya kudaiwa zimeharibika, na kumfanya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, kuamuru Kituo hicho kifungwe hadi mashine hizo zitakapoanza kufanyakazi.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiamuru Kituo cha Mafuta cha Mjimwema Kigamboni kifungwe, baada ya kubaini kuwa wamiliki wamekiuka masharti kwa kutotumia mashine maalumu za kielektroniki ya kutolea risiti hatua inayoikosesha Serikali mapato ya kodi.
 
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alipotembelea kwa kushitukiza, katika Kituo cha Mafuta cha OilCom kilichoko Kigamboni Jijini Dar es Salaam na kubaini pia kwamba kituo hicho hakijafunga mashine maalumu zinazofungwa kwenye pampu za mafuta kwa ajili ya kutolea risiti kwa wateja wake.