Home » Video » Hotuba ya Rais Mstaafu Kikwete kwenye Maadhimisho ya miaka 39 ya CCM

Hotuba ya Rais Mstaafu Kikwete kwenye Maadhimisho ya miaka 39 ya CCM

News Category: 

Kuzaliwa kwa CCM

Katika Mkutano Mkuu wa Pamoja wa TANU na ASP uliofanyika tarehe 22 Septemba, 1975 Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba Tanzania ni nchi yenye Chama kimoja;

“Lakini kwa sababu kuna vyama viwili TANU na ASP, Katiba inazungumza juu ya Chama kimoja, hicho Chama kimoja kwa kweli ni vyama viwili … Siasa ya TANU na ASP ni moja yaani Ujamaa na Kujitegemea. Midhali Katiba ya Tanzania ni ya Chama kimoja, Katiba hiyo inataka hicho Chama chenye Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kishike hatamu na uongozi wa nchi”. (Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, uk. 3-4).

Kwa msisitizo huo, Mwalimu alipendekeza kuunganishwa kwa TANU na ASP na kuundwa kwa chama kipya. Pendekezo hilo liliwasilishwa kwa wanachama wa TANU na ASP ili kujadili na kutoa maoni yao. Matokeo ya maoni ya wanachama ni kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanachama walikubaliana na pendekezo la Mwalimu Nyerere. Baada ya kupokea matokeo ya maoni ya wanachama wao, Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU na ile ya ASP, zilikutana na kufanya kikao cha pamoja Oktoba, 1976. Katika mkutano huo iliteuliwa Tume ya Watu 20 iliyopewa jukumu la kutayarisha Katiba ya Chama kipya. Mwenyekiti wa Tume hiyo alikuwa Sheikh Thabit Kombo na Katibu wake alikuwa Ndugu Pius Msekwa.

 

Wajumbe wa Tume ya Watu 20 ya kuandaa Katiba ya CCM:-

Kutoka ASP:                                                 Kutoka TANU:

1. Sheikh Thabiti Kombo                            1. Ndugu Peter A. Kisumo

2. Ndugu Ali Mzee                                      2. Ndugu Pius Msekwa

3. Ndugu A.S. Natepe                                3. Ndugu Daudi N. Mwakawago

4. Ndugu Seif Bakari                                   4. Ndugu Kingunge Ngombale-Mwiru

5. Ndugu Hamisi Hemed                             5. Ndugu Jackson Kaaya

6. Ndugu Rajab Kheri                                 6. Ndugu Peter S.Siyovelwa

7. Ndugu Asia Amour                                 7. Ndugu Nicodemus M. Banduka

8. Ndugu Hassan N. Moyo                        8. Ndugu Lawi N. Sijaona

9. Ndugu Juma Salum                               9. Ndugu Beatrice P. Mhango

10. Ndugu Hamdan Muhiddin                    10. Ndugu Basheikh A. Mikidadi

Mkutano Mkuu wa Pamoja wa vyama vya ASP na TANU uliofanyika tarehe 21 Januari, 1977 uliazimia ifuatavyo:-

“Sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa pamoja wa TANU na ASP tuliokutana leo tarehe 21 Januati, 1977 mjini Dar es Salaam, chini ya uongozi wa pamoja wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Rais wa TANU na Ndugu Aboud Jumbe, Rais wa ASP, kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari , 1977 na wakati huo huo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba” (Katiba ya CCM).

 

Aidha, Azimio hilo lilisisitiza kwamba:

“Chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vyake vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini …” (Katiba ya CCM)

Mkutano Mkuu huo wa pamoja ulipitisha pia Katiba ya CCM na kumchagua Mwalimu Nyerere kuwa Mwenyekiti wa CCM, Sheikh Aboud Jumbe kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM na Ndugu Pius Msekwa kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM.

Azma ya CCM ilikuwa ni kuendeleza mazuri yote ya TANU na ASP na kuyaacha mabaya. Miongoni mwa mazuri yaliyoendelezwa na CCM ni pamoja na:

Kuendelea kuimarisha uhuru wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar.

Kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Kuendelea kutekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Kuendelea kupanua na kuimarisha demokrasia ndani ya Chama na nchini ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya demokrasia Zanzibar. Katiba ya CCM iliwataka wanachama wake Zanzibar kuwa na viongozi wengi wa kuchaguliwa badala ya uteuzi kama ilivyokuwa chini ya ASP. Kwa kupitia Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, wananchi wa Zanzibar walipata fursa ya kwanza ya kuwachagua Wabunge wao. Aidha, kwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, Baraza la Wawakilishi liliundwa mwaka 1980 na Wawakilishi kupatikana kwa njia ya kura ya siri.

 

CCM katika kipindi cha Mageuzi:

CCM kama ilivyokuwa kwa TANU na ASP, kimeendelea kuongoza nchi yetu hata chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorejeshwa rasmi tarehe 1 Julai, 1992. Changamoto inayoikabili CCM ni kuendelea kuwa chombo cha uongozi katika mazingira haya ya mfumo wa vyama vingi vya siasa na mazingira ya utandawazi bila ya kuwepo Baba wa Taifa.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999 Jijini London katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas. Kifo cha Baba wa Taifa kilikuwa ni pigo kubwa kwa CCM na Taifa letu. Kwa Watanzania, Mwalimu ni maarufu kwa sababu yeye ndiye mwanzilishi wa Taifa letu, ni mwanzilishi wa TANU hadi kuleta uhuru; Mwalimu na Mzee Abeid Amani Karume ndio walioasisi Muungano; Mwalimu na Mzee Aboud Jumbe ndio walioasisi CCM; Mwalimu ndiye aliyelijenga na kutuachia Taifa lenye umoja, udugu na mshikamano. Afrika itamkumbuka kama kiongozi shupavu na aliyejitolea mhanga kwa ajili ya ukombozi wa Afrika. Dunia itamkumbuka Mwalimu kama mtetezi wa wanyonge wa dunia, hasa wa nchi za Kusini. La msingi katika kumkumbuka ni kuendeleza yote mema aliyotuachia.

 

Chini ya mfumo wa Vyama vingi vya siasa CCM kimeweza kufanya mageuzi makubwa ya kisiasa kiuchumi na kijamii. Mageuzi ya kiuchumi yanaendelea kwa mafanikio makubwa kupitia Ubinafsishaji na mkakati wa Uwezeshaji chini ya mkakati mkuu wa modenaizesheni. Mageuzi ya kisiasa yameibua kuanzishwa kwa vyama 16 vya siasa vilivyosajiliwa. Hata hivyo CCM kimeweza kujiimarisha kisiasa na kiuhalali kupitia ushindi wa chaguzi kuu za 1995 na 2000. Ilani ya Uchaguzi ya 2000 inaendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa. Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2003 kasi ya kukua kwa uchumi wa Tanzania umefikia asilimia 6.5 licha ya hali ya majanga kama vile ukimwi na ukame yanayotishia mafanikio hayo. Kasi hii ni ya juu katika nchi za SADC kwa kipindi hicho.

 

Aidha CCM inaendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mfumo wa vyama vingi hauwi sababu ya chuki na msambaratiko wa umoja wa kitaifa, amani na mshikamano. Katika msimamo huo CCM imeweza kufikia MUAFAKA na CUF, hatua ambayo imetoa fursa kwa Zanzibar kurejesha hali ya amani, utulivu na mashirikiano, hivyo kuweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

 

5.0 HITIMISHO:

5.1 Tunajifunza nini kutokana na historia ya TANU na ASP? Historia ya TANU na ASP inaonyesha kwamba Chama chetu wakati wote kimekuwa na sifa zifuatazo:

kuimarisha umoja;

kujenga utaifa na uzalendo;

kupanua demokrasia ndani ya chama; 

kubadilika mara kwa mara kifikra na kimuundo kulingana na wakati;

pamoja na kutambua na kushughulikia matatizo ya wananchi.

 

 

Ad